Iran yakanusha madai yasiyo na msingi kuhusu haki za binadamu
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Baghaei Hamane amesema madai yaliyotolewa na baadhi ya nchi za Magharibi kuhusu haki za binadamu Iran hayana ukweli wala ushahidi wenye mashiko.
Akizungumza Jumanne katika kikao cha 44 cha Baraza la Haki za Binadamu, Hamaneh amesema Idara ya Mahakama Iran ni huru na inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria za kimataifa na pia huzingatia mikataba ya kimataifa ambayo Iran imeitia saini.
Amesema hakuna yeyote mwenye haki ya kuilazimu Iran ibadilishe mfumo wake wa kisheria.
Aidha ameashiria uhasama wa Marekani dhidi ya Iran na kuongeza kuwa nchi za Magharibi ambazo zimetoa taarifa dhidi ya Iran ni washirika wa sera za kijinai za Marekani.
Baghaei Hamaneh amesema Iran haitumii haki za binadamu kama chombo cha kuwavutia marafiki au kuwapinga maadui.
Jana pia Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran iliyataja madai yasiyo na msingi ya nchi za Ulaya kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu nchini Iran kuwa hayana uhalali wowote wa kisheria.
Baadhi ya nchi za Ulaya hivi karibuni zimetoa taarifa yenye kukinzana katika kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na kukosoa hali ya haki za binadamu nchini Iran.