Jumanne, tarehe 18 Machi, 2025
Leo ni Jumanne tarehe 17 Ramadhani 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 18 Machi 2025.
Siku kama ya leo miaka 1447 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia Mtume Muhammad SAW alisafiri kutoka Makka hadi Baitul Muqaddas na kupaa mbinguni kwa amri ya Mwenyezi Mungu.
Aya ya kwanza ya Sura ya al Israa inatoa maelezo kuhusu muujiza huo mkubwa ikisema. "Ametakasika aliyemchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyouzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya ishara Zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona."
Kwa kuzingatia aya hiyo na Hadithi za Mtume Muhammad SAW, wakati mtukufu huyo alipokuwa katika safari ya Miiraji alionyeshwa siri nyingi za Mwenyezi Mungu SW, viumbe vyake Jalali na hatima ya wanadamu katika ulimwengu wa Akhera. Tukio hilo ni miongoni mwa miujiza mikubwa ya Mtume Muhammad SAW na linadhihirisha nafasi ya juu ya mtukufu huyo.

Siku kama ya lao miaka 212 iliyopita, alizaliwa Christian Friedrich Hebbel mwanafasihi na mkosoaji mkubwa wa Ujerumani.
Akiwa kijana mdogo na kutokana na kufariki dunia baba yake, alilazimika kufanya kazi katika kiwanda cha kuchapisha magazeti kwa lengo la kujidhaminia mahitaji yake. Hata hivyo baada ya kufanya tafiti kadhaa na kujiongezea maarifa, alianza kazi ya uandishi. Akiwa na umri wa miaka 20 Christian Hebbel alianza kusambaza Makala zake kwa ajili ya kuchapishwa katika magazeti ya fasihi ya mjini Hamburg, Ujerumani.
Baada ya hapo alijiendeleza zaidi kielimu ambapo sambamba na kuendelea na masomo pia alikuwa akijihusisha na kazi za fasihi na kuandika michezo ya sinema mbalimbali ambapo pia katika uwanja huo ameacha athari katika uga wa fasihi na nadharia za ukosoaji. Hebbel alifariki dunia mwaka 1863 Miladia akiwa na umri wa miaka 50.

Miaka 167 iliyopita katika siku kama leo, alizaliwa mvumbuzi mashuhuri wa Kijerumani, Rudolf Diesel, ambaye alibuni injini ya diseli.
Diesel alifanya utafiti na uhakiki mkubwa kuhusu injini za mitambo mbalimbali na akafanikiwa kuvumbua chombo ambacho kinaweza kuzalisha nishati kubwa zaidi bila ya kuhitaji umeme lakini kwa kutumia nishati ya kawaida na rahisi zaidi.
Chombo hicho ambacho kilipewa jina lake mwenyewe la Diesel kilileta mabadiliko makubwa katika sekta ya viwanda na usafirishaji kwa kadiri kwamba licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia lakini injini za diseli zingalia zinatumika kwa kuwa ni zenye nguvu kubwa na zinazotumia nishati ndogo. Rudolf Diesel alifariki dunia mwaka 1913.

Miaka 60 iliyopita katika siku kama ya leo, mfalme Farouk wa Misri aliyekuwa ameondolewa madarakani, aliaga dunia.
Mfalme Farouk alizaliwa 1920. Alizaliwa katika kipindi ambacho baba yake yaani Ahmad Fuad alikuwa akitawala nchini Misri kwa anuani ya Fuad wa Kwanza. Farouk alichukua madaraka akiwa na umri wa miaka 16 baada ya kuaga dunia baba yake.
Hata hivyo kutokana na kutotimiza umri wa kisheria, uongozi na usimamizi wa nchi ulikabidhiwa kwa Baraza la Niaba la Ufalme.
