Marekani yaiwekea Iran vikwazo vingine vipya vya kibenki
Serikali ya Marekani imeiwekea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vikwazo vipya vya kibenki ukiwa ni mwendelezo wa mashinikizo na vikwazo vya kidhalimu vya Washington dhidi ya Tehran.
Gazeti la Washington Post limewanukuu maafisa wa Ikulu ya White House ambao hawakutaka majina yao yatajwe wakieleza kwamba, karibuni hivi Rais Donald Trump wa Marekani atayajumuisha kwenye vikwazo majina ya benki kadhaa za Iran ambazo hapo awali hazikuwemo kwenye orodha ya vikwazo visivyo vya moja kwa moja vya Washington.
Kwa kuziwekea vikwazo zaidi ya benki 12 za Iran, serikali ya Marekani imedhamiria kupiga marufuku kufanyika mawasiliano na sekta zote za kifedha za Jamhuri ya Kiislamu.
Hatua hiyo ya Marekani inaweza ikalenga uingizaji nchini bidhaa zinazohitajika kwa masuala ya kibinadamu kama chakula na dawa.
Kabla ya hapo, Trump alitangaza amri ya utekelezaji ya kuziwekea vikwazo sekta za viwanda, ujenzi na madini za Iran.
Lengo la Trump la kuchukua hatua hiyo ya kuiwekea Iran vikwazo vikali ni kumzuia Joe Biden, mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democrat asiweze kuirejesha nchi hiyo kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA endapo atashinda katika uchaguzi wa Novemba 3.
Awali wabunge 56 wa Kongresi ya Marekani waliandika barua ya kuitaka serikali ya Donald Trump iziweke sekta zote za masuala ya fedha za Iran kwenye orodha ya vikwazo vya nchi hiyo.
Hayo yanafanyika wakati nchi 26 ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yenyewe, Syria, Russia, China na Iraq zimesisitiza kuwa vikwazo vya kidhalimu vya kiuchumi vya Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi dhidi ya nchi zenye misimamo huru duniani ni kizuizi kikubwa kwa nchi hizo kwa ajili ya kukabiliana na janga la virusi vya corona na zimetaka kukomeshwa vikwazo hivyo.
Vikwazo vya upande mmoja na vya kidhalimu vya Washington ambavyo vinajumuisha bidhaa za msingi zikiwemo hata dawa na vifaa vya tiba vimesababisha matatizo mengi kwa wananchi wa mataifa yaliyowekewa vikwazo na Marekani hususan wagonjwa wa corona.../