Kufilisika benki za Marekani na hofu ya madhara yake
https://parstoday.ir/sw/news/world-i95216-kufilisika_benki_za_marekani_na_hofu_ya_madhara_yake
Mtikisiko uliosababishwa na kufilisika kwa Benki ya Silicon Valley (SVB) unaendelea kushuhudiwa katika jamii ya Marekani. Wataalamu wengi pia wana wasiwasi kuhusu mustakbali wa uwekezaji na hali ya uchumi katika nchi hiyo na uwezekano wa hali hiyo kuhamia katika maeneo mengine, ikiwa ni pamoja na Ulaya.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 18, 2023 04:05 UTC
  • Kufilisika benki za Marekani na hofu ya madhara yake

Mtikisiko uliosababishwa na kufilisika kwa Benki ya Silicon Valley (SVB) unaendelea kushuhudiwa katika jamii ya Marekani. Wataalamu wengi pia wana wasiwasi kuhusu mustakbali wa uwekezaji na hali ya uchumi katika nchi hiyo na uwezekano wa hali hiyo kuhamia katika maeneo mengine, ikiwa ni pamoja na Ulaya.

Kufilisika kwa ghafla kwa Benki ya Silicon Valley (SVB), ambayo ilifungwa siku ya Ijumaa na mamlaka ya Marekani, kumeibua wimbi la hofu kwenye sekta ya benki nchini humo; kiasi kwamba masoko ya nchi hiyo yametumbukia katika mjadala juu ya athari mbaya za kusambaratika na kufilisika kukubwa zaidi kwa benki nchini Marekani tangu baada ya mgogoro wa kifedha wa 2008. Watu wengi pia wana wasiwasi kuhusu uwezekano wa kupanuka zaidi hali hii hadi kwenye benki nyingine, zikiwemo benki za Ulaya. Kufilisika Benki ya Silicon Valley ya Marekani pia kumepiga kengele ya hatari ya kufilisika mabenki barani Ulaya na kuzua wahka na hofu kwa serikali na makampuni ya bara hilo.

Baada ya tangazo la kufilisika Benki ya Silicon Valley, Rais wa Merekani, Joe Biden alijaribu kuwahakikishia wawekezaji katika benki hiyo kwamba rasilimali zao zitalindwa; hata hivyo, hali ya kiuchumi ya Marekani inaonyesha kuwa utawala wa Biden haujaweza kuwapa matumaini na dhamana ya kutosha wawekezaji katika benki za nchi hiyo.

Lawrence Summers, waziri wa zamani wa fedha ya Marekani, anasema: "Kufilisika kwa Benki ya Silicon Valley kutakuwa na matokeo mengi mabaya kwa uchumi wa Marekani. Serikali ya Marekani lazima iwahakikishie watu wote kwamba itaondoa tatizo hili."

Kabla ya kufilisika, Benki ya Silicon Valley ilikuwa mfadhili wa nusu ya makampuni ya teknolojia ya Marekani. Kufilisika kwa benki hiyo pia kumesababisha mtikisiko na matatizo duniani kote. Kwa mfano, kampuni kadhaa za Brazil ambazo zilikuwa zimewekeza dola bilioni 10 katika benki hiyo zimepoteza pesa zao. Hii ni sehemu ndogo tu ya matatizo. Kampuni nyingi za India, Uchina na Ulaya pia zimepoteza mitaji yao katika kufilisika kwa Benki ya Silicon Valley. Hali hii inakumbusha kufilisika kwa benki kubwa zaidi katika mgogoro wa kiuchumi wa 2008, ambao ulisababisha mdororo mkubwa wa uchumi wa dunia.

Sababu mbalimbali zimetajwa za kufilisika Benki ya Silicon Valley ikiwa ni pamoja na mdororo wa uchumi wa Marekani. Sababu nyingine ni kwamba mwaka jana, Federal Reserve (Benki Kuu ya Marekani) iliinua juu viwango vya riba ili kupunguza mfumuko wa bei. Kufuatia uamuzi huo, hisa za kampuni zinazofanya kazi katika uwanja wa teknolojia ya kisasa, ambazo zilikuwa na sehemu kubwa ya uwekezaji katika Benki ya Silicon Valley, zilipoteza thamani.

Wakati huo huo, Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani amemtaja Joe Biden, rais wa sasa wa nchi hiyo, kuwa ndiye anayehusika na matatizo ya kiuchumi ya Marekani. Akiashiria mdororo mkubwa wa kiuchumi unaoinyemelea Marekani, Trump amesema: Tutakuwa na mdororo mkubwa na wenye nguvu kubwa zaidi ya mdororo wa 1929, na mchakato wa kufilisika kwa benki tayari umeanza.

Wachambuzi wengine wengi waanaamini kuwa, serikali ya Biden imezingatia zaidi masuala ya kijiopolitiki na ya nje ya nchi badala ya kutilia maanani masuala ya ndani ya Marekani, na hii imesababisha kupuuzwa masuala ya ndani.

Joe Biden akiwa Kiev kuunga mkono serikali ya Ukraine katika vita vyake na Russia

Wako watu wengi ambao hawaioni hali ya sasa ya uchumi wa Marekani kuwa si sawa na hali ya huko nyuma na wanachukulia hali ya sasa kuwa ya muda na kwamba athari zake zinaweza kupunguzwa kwa hatua za serikali. Mshauri wa kiuchumi wa Ikulu ya White House, Cecilia Rouse, anasema: Tuko katika hali tofauti kabisa ikilinganishwa na mageuzi yanayohusiana na mgogoro wa kifedha duniani mwaka 2007 na 2008.

Pamoja na hayo yote, kufilisika kwa Benki ya Silicon Valley kumesababisha hasara kubwa kwa kampuni zinazofanya kazi katika sekta ya teknolojia ulimwenguni. Inaonekana kuwa katika wiki zijazo, kutaibuka mambo mengi zaidi ya kiuchumi ambayo yanayotokana na taathira mbaya za kufilisika Benki ya Silicon Valley.