Benki za Kiislamu Tanzania zakumbatiwa na wasiokuwa Waislamu
Benki za Kiislamu nchini Tanzania zimeendelea kupata umaarufu na kupongezwa kwa huduma zao, na sasa zinawavutia kwa wingi hata wateja wasiokuwa Waislamu nchini humo.
Hayo yameripotiwa na shirika la habari la Anadolu ambalo limeeleza kuwa, maadili na utendaji kazi wa benki hizo zinazofuata mfumo wa kibenki wa Kiislamu ni miongoni mwa sababu za benki hizo kukumbatiwa na hata wasiokuwa Waislamu nchini Tanzania.
Kinyume na benki au mashirika mengine ya kifedha, mashirika ya kifedha ya Kiislamu huwa hayatozi riba kwa mikopo na pia hujizuia kuwekeza fedha za wateja katika sekta au huduma ambazo ni haramu kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu kama vile pombe, kamari, uuzaji wa nyama ya nguruwe nk.
Waislamu wanajenga asilimia 35 ya jamii yote ya Watanzania ambao ni milioni 59.05. Nchi hiyo ya Afrika Mashariki ilitangazwa rasmi kuwa nchi ya kipato cha kati mwaka juzi 2020.
Miraji Athumani, Mkuu wa Kitengo cha Benki ya Kiislamu ndani ya Benki ya Biashara ya Tanzania (TCB) ambayo huko nyuma ilifahamika kama Tanzania Postal Bank (TPB) ameiambia Anadolu kuwa, hatua ya benki hiyo kutumia fedha za wateja kuwekeza katika biashara na kisha kuwapa wateja hao faida badala ya riba, imepelekea taasisi hiyo ya fedha kupendwa na hata Watazania wasiokuwa Waislamu.

Athumani amebainisha kuwa, "Wateja wetu wanafurahi kujua kuwa pesa zao zipo katika mikono salama, na wala haziwekezwi kinyume na matamanio na maazimio yao."
Kenya, Tanzania na Ethiopia ni miongoni mwa nchi za Kiafrika zenye benki na taasisi nyingine za kifedha zinazofuata mafundisho ya Kiislamu. Benki za Kiislamu zinaonekana kuwa kivutio kwa wateja wengi kutokana na uwajibikaji wake unaoenda sawa na mafundisho ya Kiislamu.