Maomblezo ya kuaga dunia Mtume (saw) na kuuawa shahidi Imam Hassan (as)
(last modified Fri, 16 Oct 2020 07:22:40 GMT )
Oct 16, 2020 07:22 UTC
  • Maomblezo ya kuaga dunia Mtume (saw) na kuuawa shahidi Imam Hassan (as)

Taifa zima la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limezama katika maombolezo ya kumbukumbu ya kuaga dunia Mtume Mtukufu wa Uislamu (saw) pamoja na kuuawa shahidi Imam Hassan Mujtaba (as), Imam wa pili wa Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Leo Ijumaa tarehe 28 Swafar 1442 sawa na tarehe 16 Oktoba 2020 ni siku ya kukumbuka kuaga dunia Mtume Mtukufu (saw) na Imam Hassan bin Ali al-Mujtaba (as), ambaye ni Imam wa pili wa Mashia duniani.

Kabla ya kuaga kwake dunia mwaka wa 11 Hijiria, Mtume (saw) alifanya juhudi kubwa na kupitia machungu na mateso mengi kutoka kwa makafiri wa Makka katika kuwafikishia watu ujumbe wa mafundisho ya dini tukufu ya Uislamu.

Alikuwa na subira na kuonyesha huruma kubwa katika njia hiyo ya kuwatoa wanadamu kwenye giza la upotevu na ujahili na kuwaongoza kwenye njia ya wokovu na saada ya kudumu milele.

Imam Hassan Mujtaba (as) ambaye alikuwa chini ya malezi ya baba yake Imam Ali (as), Imam wa kwanza wa Mashia, kwa muda wa karibu miaka 30 pia alifanya juhudi kubwa za kuwaongoza Waislamu katika njia ya dini ya babu yake, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw).

Alipewa sumu na mke wake kwa amri na njama ya mtawala dhalimu Muawiya, na kuaga dunia katika tarehe kama ya leo mwaka wa 50 Hijiria, akiwa na umri wa miaka 47.

Kwa mnasaba huu mchungu wa kukumbuka kuaga dunia Mtume Mtukufu (saw) pamoja na kuuawa shahidi mjukuu wake mwema Imam Hassan al-Mujtaba (as), Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani na hasa wapenzi wa Ahlul Bait wa Mtume (saw).