Mkutano wa 34 wa kimataifa wa Umoja wa Kiislamu kufanyika Tehran
Mkutano wa 34 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu unatazamiwa kuanza Alhamisi katika mji mkuu wa Iran, Tehran ambapo mada kuu itakuwa 'Ushirikiano wa Kiislamu Wakati wa Maafa na Majanga'.
Akizungumza na waandishi habari hivi leo mjini Tehran, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu Hujjatul Islam Hamid Shahriyari amesema kongamano hilo litaanza Alhamisi na kuendelea hadi Jumanne ijayo yaani tarehe tatu Novemba. Agha;abu ya vikao hivyo vitafanyika kwa njia ya intaneti ili kuzuia maambukizi ya corona.
Hujjatul Islam Hamid Shahriyari ameongeza kuwa, Kongamano la 34 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu mwaka huu litakuwa na wazungumzaji 167 wa kigeni kutoka nchi 47 na 120 kutoka Iran. Amesema wazungumzaji ni wanazuoni na wasomi maarufu kutoka ulimwengu wa Kiislamu na wataalamu wa masuala ya umoja na kukurubisha madhehebu za Kiislamu.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu amesema katika kongamano la mwaka huu kutazinduliwa vitabu viwili kuhusu Palestina sambamba na kufunguliwa Radio ya Umoja.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu aidha ameashiria kitendo cha wakuu wa Ufaransa kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW na kusema: "Maadui wanahimiza chuki dhidi ya Uislamu na hivyo kuna haja ya kutumia busra na mazungumzo ili kuwasilisha Uislamu halisi duniani na tusiruhusu hao maadui wauarifishe Uislamu ambao si sahihi ambao unahimiza machafuko kwa lengo la kuchafua jina la Uislamu halisi."
Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu hufanyika kila mwaka kwa munasaba wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu. Inafaa kuashiria hapa kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni kipindi cha kati ya tarehe 12 na 17 za Mfunguo Sita Rabiu Awwal kipindi ambacho kinasadifiana na kuadhimisha Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Bwana Mtume SAW.