Zarif: Ziara yangu Venezuela imekuwa na mafanikio makubwa
(last modified Fri, 06 Nov 2020 06:38:11 GMT )
Nov 06, 2020 06:38 UTC
  • Zarif: Ziara yangu Venezuela imekuwa na mafanikio makubwa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kuhusu ziara yake nchini Venezuela akiashiria jinsi ziara yake hiyo ilivyofanyika kwa ufanisi mkubwa.

Mapema leo Ijumaa, Dk Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameweka picha za mazungumzo yake na viongozi wa ngazi za juu wa Venezuela na kuandika: Nchini Venezuela nimeonana na Rais Nicolas Maduro pamoja na makamu wa rais wa nchi hiyo, Delcy Rodríguez na Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela, Jorge Arreaza, na tumejadiliana masuala muhimu ya kustawisha uhusiano wa pande mbili. 

Aidha ameandika: Katika taasisi ya Samuel Robinson nimetoa hotuba kuhusu njama za Marekani na Magharibi za kuzusha hofu kwa nia ya kukwamisha njia ya kihistoria ya ulimwengu wa baada ya Magharibi.

Zarif akiwa ziarani nchini Venezuela

 

Juzi Jumatano, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliwasili katika eneo la Amerika ya Latini kwa ajili ya ziara rasmi ya kuzitembelea nchi za Cuba, Bolivia na Venezuela. Ziara yake hiyo imeanzia nchini Venezuela.

Jana Alkhamisi alionana na waziri mwenzake wa Venezuela, Jorge Arreaza na akaipongeza Caracas kwa uimara wake katika kukabiliana na siasa za kibeberu za Marekani. Alisema katika mazungumzo hayo kwamba zama za mabavu ya nchi za Magharibi zimeisha.

Jana pia alionana na Rais Nicolas Maduro ambapo rais huyo wa Venezuela alimpokea kwa mapenzi na shauku kubwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran. 

Tags