Ghalibaf: Vikwazo vya Marekani dhidi ya nchi huru, ni siasa zilizofeli
(last modified Tue, 24 Nov 2020 02:24:13 GMT )
Nov 24, 2020 02:24 UTC
  • Ghalibaf: Vikwazo vya Marekani dhidi ya nchi huru, ni siasa zilizofeli

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, vikwazo vya Marekani dhidi ya nchi huru duniani ni siasa zilizofeli na kuongeza kuwa, vikwazo hivyo vimeimarisha misingi ya uchumi wa kutengemea uwezo wa ndani, nchini Iran.

Mohammad Bagher Ghalibaf alisema hayo jana wakati walipoonana na Balozi wa Uturuki hapa Tehran, Bw. Derya Örs na huku akigusia uhusiano wa jadi na imara baina ya Iran na Uturuki amesema, katika miaka ya hivi karibuni na licha ya kuweko vikwazo vya kidhulma vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, lakini misingi na nguzo za uzalishaji wa ndani ya Iran zimezidi kuwa imara na taifa la Iran limeweza kubadilisha vitisho kuwa fursa za kujiletea maendeleo imara yasiyoyumba.

Spika wa Bunge la Iran vile vile amesema kwamba nchi mbili ndugu za Kiislamu, yaani Iran na Uturuki zinapaswa kuimarisha zaidi na zaidi ushirikiano wao wa kiuchumi hasa wakati huu wa kipindi cha kuenea wimbi la ugonjwa wa COVID-19. Amesema, kadiri uhusiano wa nchi hizi ndugu jirani unavyozidi kustawi, ndivyo zinavyojitokea fursa nzuri zaidi za kushirikiano wa pande zote na kuna wajibu wa kutumia vizuri rusa hizo kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizi mbili.

Bendera za Iran na Uturuki, ishara ya uhusiano mzuri baina ya nchi mbili

 

Kwa upande wake, Balozi wa Uturuki hapa Tehran, Derya Örs ameunga mkono msimamo wa Spika wa Bunge la Iran kuhusu masuala yote aliyoyagusia katika mazungumzo hayo yakiwemo ya ushirikiano wa mabunge ya nchi hizo mbili na kuongeza kuwa, mabunge ya nchi hizi mbili yanapaswa kuimarisha ushirikiano wao kadiri inavyowezekana .

Vile vile amehimiza kuondolewa haraka vizuizi vyote vinavyoweza kujitokeza, na kuimarisha uhusiano wa nchi mbili kwa kiwango cha juu sana.