Iran yazipongeza Pakistan na India kwa kulinda usimamishaji vita
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa Tehran inazipongeza Pakistan na India kwa tamko lao la pamoja la kuyalinda makubaliano ya kusimamisha vita na kusema kuwa hiyo ni hatua nzuri ya kuelekea kwenye amani na utulivu wa kudunu katika eneo la kusini mwa Asia.
Saeed Khatibzadeh alisema hayo jana na kuongeza kuwa, taarifa ya pamoja baina ya India na Pakistan inayohusiana na maafikiano yaliyofikiwa baina ya nchi hizo mbili kuhusu kulindwa na kutekelezwa kikamiifu makubaliano ya kusimamisha vita ni hatua muhimu sana ambayo ni lazima ipongezwe.
Amesema hatua hiyo ya Pakistan na India ni muhimuu sana kwa ajili ya kuleta amani na utulivu zaidi katika eneo la kusini mwa Asia na ameelezea matumaini yake kwamba nchi hizo mbili zitachukua hatua kubwa zaidi katika siku za usoni kwa ajili ya kuimarisha amani, utulivu na ustawi kwenye eneo hili lote.
Kwa mara ya kwanza baada ya miongo mwili, India na Pakistan siku chache zilizopita zilifikia makubaliano ya kusimamisha vita katika eneo la Kashamir zinaloligombania.
Mwaka 2003 nchi hizo mbili zilitiliana saini makubaliano ya kusimamisha vita katika mstari wa udhibiti huko Kashmir. Hata hivyo tangu wakati huo, nchi hizo mbili kila moja imekuwa ikiituhumu mwenzake kuwa haiheshimu makbaliano hayo.
Kadhia ya Kashmir ni miongoni mwa masuala muhimu sana yenye mzozo baina ya India na Pakistan. Vita kadhaa vimeshatokea baina ya nchi hizo mbili kuhusu eneo hilo, kutokana na kila moja kati ya Pakistan na India kudai Kaskhir ni mali yake.
Pakistan imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa kuitishwe kura ya maoni ya kuulizwa wakazi wa Kashmir wanataka kujiuunga na upande gani imma wa Pakistan au India, hata hivyo serikali zote zinazoingia madarakani huko India zimekuwa zikipinga pendekezo hilo la Pakistan.