Iran: Hatutofanya mazungumzo tena kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA
(last modified Mon, 15 Mar 2021 09:54:58 GMT )
Mar 15, 2021 09:54 UTC
  • Iran: Hatutofanya mazungumzo tena kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran haitofanya tena mazungumzo kuhusu mapatano ya kimataifa ya nyuklia yanayojulikana kwa jina la Mpango wa Pamoja wa Utekelezaji kwa kifupi JCPOA.

Televisheni ya al Alam imemnukuu Dk Mohammad Javad Zarif akisema hayo na kuongeza kuwa, Marekani inaendelea kukwamisha utekelezaji wa makubaliano hayo. Amesema, inachotakiwa kufanya Marekani ni kurejea tu kwenye mapatano hayo si kutoa matamshi isiyoyatekeleza.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amesema, Marekani imeizuia Korea Kusini kuilipa Iran fedha zake kupitia benki za Uswisi na huo ni ukwamishaji wa wazi kabisa unaofanywa na Washington dhidi ya Iran.

Amesisitiza kuwa, rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump alisimamisha miamala yote na Iran. Serikali ya hivi sasa ya Joe Biden huko Marekani inapaswa kurejea kwenye mapatano ya nyuklia na itambue kuwa Iran kawe haitorudi kwenye mazungumzo kuhusu maudhui ambazo huko nyuma zilijadiliwa kwa kina na kufikiwa makubaliano ya pande zote.

Bunge la Iran lilipasisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA ili kuyapa nguvu za kisheria

 

Amesisitiza kuwa, Tehran haitaki chochote kilichoko nje ya makubaliano ya JCPOA na kwamba Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA wenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa mapatano hayo, umethibitisha mara chungu nzima kwamba Tehran imeheshimu kikamilifu makubaliano hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha ameonya kwa kusema: Tunaishauri Marekani ichukue haraka hatua za kuimarisha mapatano hayo kabla ya kutoweka fursa iliyopo.

Aidha amesema, hatua ya Iran ya kurutubisha urani kwa kiwango cha asilimia 20 imefanyika kwa malengo ya amani kikamilifu. Amesema: Sisi hatuna haja na silaha za nyuklia na haiwekezakani kabisa kwetu kutumia silaha hizo za maangamizi ya umati.

Tags