Jul 21, 2024 06:49 UTC
  • Blinken: Kujiondoa JCPOA ni katika makosa makubwa ya Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amekiri bayana kuwa, hatua ya nchi hiyo ya kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni moja ya makosa makubwa zaidi yaliyowahi kufanywa na Washington katika miaka ya hivi karibuni.

Antony Blinken amesema hayo katika Mkutano wa Usalama wa Aspen na kueleza kuwa, "Moja ya makosa makubwa tuliyofanya katika miaka ya karibuni, ni kutupilia mbali makubaliano hayo (ya nyuklia), na kuiruhusu Iran iondoke nje ya kijisanduku tulipoiweka."

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Marekani amedai kuwa, kwa kujiondoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa, Marekani imepunguza muda unaohitajika na Iran kuzalisha silaha ya nyuklia, kutoka angalau mwaka mmoja, hadi wiki moja au mbili.

Hii ni katika hali ambayo, Jamhuri ya Kiislamu mara chungu nzima imesisitiza kuwa haina nia ya kuunda silaha za nyuklia, na inachofuatilia siku zote ni nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani.

Weledi wa mambo wanaitaka Marekani iiondolee vikwazo sekta ya mafuta ya Iran ili makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambayo Washington ilijiondoa kwayo Mei mwaka 2019 yaendelee kutekelezwa.

Serikali Rais Joe Biden wa Marekani licha ya kukiri kufeli sera za mashinikizo ya kiwango cha juu za serikali ya kabla yake dhidi ya Iran, lakini mpaka sasa haijachukua hatua ya maana ya kuirejesha Washington katika mapatano hayo ya kimataifa.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa upande wake inasisitiza kuwa, kwa kuzingatia kuwa Marekani ndio mkiukaji mkuu wa JCPOA, ni Washington ndiyo inapaswa kurejea katika mapatano hayo kwa kuondoa vikwazo na kutekeleza wajibu wake kwenye mapatano hayo.

Tags