Mar 16, 2021 08:04 UTC
  • Wanadiplomasia Tehran washiriki katika sherehe za mwaka mpya wa Kiirani, Nowruz

Mabalozi na wawakilishi wa zaidi ya nchi 80 na pia wawakilishi wa taasisi za kimataifia nchini Iran wameshiriki katika maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiirani Nowruz ambao unatazamiwa kuanza Machi 21.

Kwa mujibu wa taarifa, sherehe hiyo iliyofanyika chini ya anwani ya "Nowruz 1400" ilifanyika Jumatatu alasiri katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na kuhudhuriwa pia na mawaziri kadhaa wa Iran akiwemo waziri wa mambo ya nje, waziri wa sayansi na teknolojia,  waziri wa utamaduni na waziri wa utalii.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif allitoa salamu zake za kheri na fanaka kwa kuwadia mwaka mpya wa Kiirani wa Hijria Shamsiya.

Amesema siku kuu ya Nowruz ni siku kuu ya kimataifa na kuongeza kuwa karne ya 14 iliyomalizika ya Hijria Shamsiya iligubikwa na vita, vikwazo na ubaguzi dhidi ya jamii ya mwanadamu. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameelezea matumaini kuwa, karne mpya ya 15 Hijria Shamsiya itakuja na matumaini ya kumalizika majanga ya kimaumbile, magonjwa vita na vikwazo. 

Mabalozi wa nchi za kigeni wakiwa katika sherehe za Nowruz zilizofanyika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Machi 15 2021

Mwaka 2010 Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi tarehe Mosi Farvardin, ambayo huwa siku ya kwanza ya mwaka wa Hijria Shamsiya kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nowruz. Siku hii kwa kawaida husadifiana na Machi 21. Umoja wa Mataifa umeitambua Siku ya Nowruz kama siku kuu ya kale ambayo huadhimishwa wakati wa kuwadia msimu wa machipuo na kuhuishwa tena mazingira.

 

Tags