Mar 21, 2025 03:27 UTC
  • Ijumaa, tarehe 21 Machi, mwaka 2025

Leo ni Ijumaa tarehe 20 Ramadhani 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 21 Machi mwaka 2025.

Leo ni tarehe Mosi Farvardin mwaka mpya wa 1404 Hijria Shamsia ambayo inasadifiana na siku ya kwanza ya mwaka wa Kiirani maarufu kwa jina la Sikukuu ya Nowruz.

Nowruz ni moja kati ya sherehe za kale zaidi duniani na ilianza kusherehekewa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Mbali na Iran nchi ambazo husherehekea Nowruz ni Afghanistan, Jamhuri ya Azerbaijan, Albania, Kyrgyzstan, Turkmenistan, Macedonia, India, Uturuki, Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia, Sudan na Zanzibar nchini Tanzania.

Mwaka 2010 Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi Machi 21 (yaani tarehe Mosi Farvardin) kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nowruz.

Umoja wa Mataifa umeitambua Siku ya Nowruz kama sikukuu ya kale ambayo huadhimishwa wakati wa kuwadia msimu wa machipuo na kuhuishwa tena mazingira. 

Siku kama ya leo miaka 1438 iliyopita sawa na tarehe 20 Ramadhani mwaka wa 8 Hijiria, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, jeshi la Kiislamu lililokuwa na wapiganaji elfu kumi chini ya uongozi wa Mtume Muhammad (saw) liliukomboa mji wa Makka.

Mtume Mtukufu alichukua hatua hiyo baada ya makafiri kukiuka makubaliano ya amani ya Hudaibiya ambayo yalisainiwa mwaka wa Sita Hijria kati yake na wakuu wa Makuraishi. Mtume Muhammad (saw) alitoa msamaha kwa wakazi wote wa Makka baada ya kukombolewa mji huo katika hali ambayo huko nyuma watu hao walikuwa wakipinga na kupiga vita Uislamu na pia walimuudhi mno Mtume na kuwatesa Waislamu. Mwenendo huo wa huruma na upendo wa Mtume (saw) uliwavutia watu wa kabila la Kuraishi na kuwafanya waingie kwa wingi katika dini tukufu ya Uislamu. Kwa msingi huo mji wa Makka ulikombolewa pasina kuwepo umwagaji damu.   

Siku kama ya leo miaka 820 iliyopita, sawa na tarehe 20 Ramadhani mwaka 626 Hijiria, alifariki dunia Yaqut Hamawi mmoja wa waandishi na wasomi tajika wa Kiislamu wa karne ya Saba Hijria na alikuwa mtaalamu mashuhuri wa jiografia.

Alizaliwa mwaka 539 Hijria huko Baghdad ambapo ujanani mwake alikamatwa mateka na kufanywa mtumwa. Hata hivyo baada ya kupita muda mfanyabiashara mmoja wa Baghdad alimnunua Hamawi na baadaye akamuachia huru.

Miongoni mwa athari za uandishi za Yaqut Hamawi tunazoweza kuziashiria ni vitabu vyake viwili alivyovipa majina ya "Mu'jamul-Buldan" na Mu'jamul- Udabaa." 

Siku kama ya leo miaka 257 iliyopita inayosadifiana na 21 Machi 1768, alizaliwa Joseph Baron Fourier mwanahisabati na mwanafizikia mashuhuri wa Ufaransa.

Baron Fourier alikuwa ni miongoni mwa wahadhiri wa mwanzoni kabisa waliofundisha somo la hesabati mara baada ya kuanzishwa Chuo Kikuu cha Paris.   

Joseph Baron Fourier

Katika siku kama hii ya leo miaka 100 iliyopita barua rasmi za serikali ya Iran zilianza kuandikwa kwa kutumia tarehe ya mwaka wa Hijria shamsia kufuatia azimio lililopasishwa na Bunge la Taifa.

Kwa utaratibu huo kalenda ya Iran ilibadilika kutoka mwaka wa Hijria Qamaria na kuwa Hijria Shamsia. Mwanzo wa miaka hiyo miwili ya Qamaria na Shamsia ni mmoja yaani hijra na tukio la kuhama Mtume (saw) kutoka Makka na kwenda Madina katika mwaka wa 13 baada ya kupewa utume (mwaka 622), lakini mwaka wa Qamaria unahesabiwa kwa kuzunguka mwezi mara 12 kandokando ya sayari ya dunia, na mwaka wa Shamsia unahesabiwa kwa dunia kuzunguka jua mara moja.

Kwa kuwa mwaka wa Hijria Shamsia una siku 365, kila mwaka huwa na siku 11 zaidi ya mwaka wa Hijria Qamaria ambao huwa na siku 354.   

Miaka 59 iliyopita katika siku kama ya leo, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) liliitangaza siku ya mauaji ya umati dhidi ya wazalendo weusi nchini Afrika Kusini yaliyotokea mwaka 1960 kuwa "Siku ya Kimataifa ya Kufuta Ubaguzi wa Rangi".

Waafrika weusi wapatao 69 waliuawa na wengine 180 kujeruhiwa katika siku kama ya leo, baada ya askari makaburu kuwafyatulia risasi watu hao waliokuwa wakiandamana kwa amani huko Sharpeville nchini Afrika Kusini kupinga siasa za ubaguzi wa rangi.

Japokuwa sera za ubaguzi wa rangi zimefutwa nchini Afrika Kusini lakini ubaguzi na ukosefu wa usawa vingali vinashuhudiwa katika sura mbalimbali kwenye maeneo mbalimbali ya dunia hususan katika nchi za Magharibi. 

Miaka 57 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitokea mapigano makubwa kati ya harakati ya PLO ya Palestina na majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika mji wa Karama ulioko Jordan.

Kwa uchache wanajeshi 1,230 wa Kizayuni waliangamizwa na makumi ya vifaru kutekelezwa au kuchukuliwa ngawira na wanamapambano wa Kipalestina kwenye mapigano hayo. Harakati ya PLO ilianza kupoteza hadhi yake ya kimapambano baada ya kulegeza misimamo yake ya kimapinduzi mwaka 1991 na kukubali kuketi kwenye meza ya mazungumzo ya amani na utawala ghasibu wa Israel; mazungumzo ambayo hayajawa na matunda yoyote kwa wananchi wa Palestina. 

Na tarehe 21 Machi 1990, nchi ya Namibia ilipata uhuru na kujitenga na Afrika Kusini.

Mwishoni mwa karne ya 19, wakoloni wa Kijerumani, Uingereza na Ureno walianza kuvutana kwa minajili ya kudhibiti na kupora utajiri na maliasili za Namibia.

Uhuru wa Namibia ulipatikana kutokana na mapambano ya harakati ya SWAPO chini ya uongozi wa Sam Nujoma.