Mapambano yamezuia kusahaulika kadhia ya Quds
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i69796-mapambano_yamezuia_kusahaulika_kadhia_ya_quds
Mkuu wa Kongamano la Pili la Kimataifa la Quds Tukufu amesema Marekani ilijaribu kusambaratisha kadhia ya ukombozi wa Quds (Jerusalem) kupitia njama mpya katika eneo lakini imefeli kutokana na kuwepo mhimili wa muqawama au mapambano ya Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 05, 2021 07:09 UTC
  • Mapambano yamezuia kusahaulika kadhia ya Quds

Mkuu wa Kongamano la Pili la Kimataifa la Quds Tukufu amesema Marekani ilijaribu kusambaratisha kadhia ya ukombozi wa Quds (Jerusalem) kupitia njama mpya katika eneo lakini imefeli kutokana na kuwepo mhimili wa muqawama au mapambano ya Kiislamu.

Katika mahojiano na Iran Press pembizoni mwa Kongamano la Pili la Kimataifa la Quds Tukufu mjini Qum, Ayatullah Alireza Arafi amesema Wamarekani waliunda kundi la kigaidi la ISIS au Daesh kwa lengo la kubadilisha mlingano wa nguvu katika eneo. Aidha amesema ule mpango wa kushinikiza nchi za Kiarabu zianzishe uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel zimefanyika kwa lengo hilo hilo hilo lakini mipango hiyo haikufanikiwa kutokana na uwepo athirifu wa harakati za mapambano ya Kiislamu.

Ayatullah Arafi aidha amesema kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds katika IRGC, kulifanyika kwa lengo la kusambaratisha mhimili wa muqawama lakini ukweli ni kuwa kuuawa shahidi makamanda wa harakati ya muqawama kumeimarisha zaidi harakati hiyo.

Aidha ametoa wito kwa Umma wa Kiislamu hasa vijana kusimama kidete kukabiliana na njama za kuanzishwa uhusiano baina ya nchi za Kiarabu na utawala haramu wa Israel kwani utawala huo ni adui nambari moja wa ulimwengu wa Kiislamu.

Kongamano la Pili la Kimataifa la Quds Tukufu limefanyika kwa njia ya intaneti kukiwa na washiriki kutoka nchi mbali mbali.

Kwa mujibu wa taarifa, kongamano hilo la siku mbili ambalo lilianza Jumanne Mei nne limemalizika leo na limehudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi zaidi ya 30. Kongamano hilo limefanyika kwa njia ya intaneti kutokana na janga la COVID-19.

Kati ya mada kuu ambazo zinajadiliwa katika kongamano hilo ni pamoja na "Palestina na Haki za Binadamu",'Njama za Utawala wa Israel katika kuikalia Quds Tukufu kwa Mabavu', 'Maazimio ya Umoja wa Mataifa Kuhusu Quds Tukufu' na 'Palestina na Umma wa Kiislamu."