May 28, 2021 12:47 UTC
  • Rais Rouhani: Tunatumai uhusiano wetu na Ethiopia utaimarika zaidi

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema anatumai kuwa uhusiano wa pande mbili wa nchi hii na Ethiopia utaboreka na kuimarika zaidi.

Rais Rouhani amesema hayo katika ujumbe aliomtumia mwenzake wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde, kwa mnasaba wa Siku ya Kitaifa ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Katika ujumbe huo, Dakta Rouhani amesema: Tunatumai kuwa, katika mwaka huu, unaosadifiana na mwaka wa 50 wa utekelezwaji wa mapatano ya uhusiano wa kirafiki baina ya Tehran na Addis Ababa, uhusiano wa nchi mbili hizi utapanuka hata zaidi.

Kadhalika Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mbali na kumtakia kila la kheri mwenzake wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde, amelitakia ufanisi taifa hilo la Pembe ya Afrika.

Ikumbukwe kuwa, siku kama ya leo miaka 30 iliyopita sawa na tarehe 28 Mei mwaka 1991, utawala wa kikomunisti wa Mengistu Haile Mariam ulisambaratika nchini Ethiopia na kupelekea mtawala huyo dikteta kukimbia nchi.

Bendera za Iran na Ethiopia

Siku hii inatambulika kama Siku ya Kitaifa nchini Ethiopia, na huadhimishwa kwa ajili ya kusherehekea kuanguka 'utawala wa kidikteta wa Derg' uliotawala baina ya mwaka 1974 na 1991.

Mfalme wa mwisho kuitawala Ethiopia alikuwa Haile Selassie ambaye aliitawala nchi hiyo tangu mwaka 1930 hadi 1974 na akapinduliwa na watawala wa kikomunisti, ambao nao baadaye walikabiliwa na upinzani mkubwa wa ndani kutokana na majanga ya njaa na matatizo mengine yaliyotokana na utawala mbaya.

Tags