Jun 30, 2021 11:06 UTC
  • Rais Rouhani: Biden anawasaliti wananchi wa Marekani

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema iwapo Rais Joe Biden wa Marekani atafeli kutekeleza makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kama alivyoahidi, basi atakuwa amewasailiti wananchi wa Marekani ambao walimpigia kura wakitaka kuona mabadiliko ya sera ghalati dhidi ya Iran za mtangulizi wake, Donald Trump.

Rais Hassan Rouhani amesema hayo leo Jumatano katika mkutano wa Baraza la Mawaziri na kufafanua kuwa, ingawaje utawala wa sasa wa Marekani unadai kuwa umeachana na mienendo na sera za vikwazo za Trump dhidi ya Iran, lakini ukweli wa mambo ni kuwa, jinai na ugaidi wa kiuchumi wa Trump ungali unatekelezwa.

Dakta Rouhani ameeleza bayana kuwa, madai dhidi miradi ya nyuklia ya Iran hayana msingi wowote, na kwamba mapatano ya nyuklia yanayofahamika kama JCPOA ni waraka unaoshiria ukweli kwamba, Iran haina haja ya kuzalisha silaha za nyuklia.

Amebainisha kuwa "taifa la Iran hii leo linakabiliana na ugaidi mwingine (wa kiuchumi) na katika kipindi cha miaka mitatu na nusu iliyopita, tumeingia katika vita vingine vya kiuchumi."

Rais wa Iran ameongeza kuwa, hatua za Trump dhidi ya Iran zilikuwa zaidi ya vita, kwa kuwa vita vina muundo, na hakuna mtu yoyote (wakati wa vita) huwashambulia wagonjwa wa saratani na wazee.

Ugaidi wa kiuchumi wa US dhidi ya Iran

Amesisitiza kuwa, iwapo Biden ataendelea kutekeleza sera hizo za kikatili za mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya taifa la Iran, basi atakuwa amesaliti kura za taifa lake mwenyewe.

Kwengine katika hotuba yake, Dakta Rouhani amebainisha kuwa, vikwazo vya Marekani na janga la Corona ndiyo mambo mawili yaliyochangia pakubwa kwa changamoto za kiuchumi wanazokabiliana nazo wananchi wa Iran hivi sasa.

Tags