Kuhuishwa JCPOA kunategemea maamuzi magumu ya Marekani na Ulaya
(last modified Sat, 03 Jul 2021 02:45:37 GMT )
Jul 03, 2021 02:45 UTC
  • Kuhuishwa JCPOA kunategemea maamuzi magumu ya Marekani na Ulaya

Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema sasa wakati umewadia kwa Marekani na nchi tatu za Ulaya kuchukua maamuzi magumu kwa ajili ya kuanza kufungamana tena kikamilifu na mapatano ya kimataifa ya nyuklia, JCPOA.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Usalama kilichoandaliwa kwa ajili ya kuchunguza ripoti za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu JCPOA na utekelezaji wa azimio nambari 2231 la baraza hilo, Majid Takht Ravanchi amesema Iran imethibitisha kivitendo ukweli wake iwe ni katika kipindi cha kufanyika mazungumzo ya JCPOA au wakati wa kutiwa saini na kutekelezwa mapatano hayo muhimu ya kimataifa.

Baada ya Rais Joe Biden kuingia White Hosue, serikali ya Washington ilichukua uamuzi wa kurejea katika mapatano ya JCPOA ambapo mazungumzo ya Vienna yalianza kufanyika ili kufikia lengo hilo. Kufikia sasa duru 6 za mazungumzo hayo zimefanyika lakini Marekani imeshindwa kuchukua uamuzi mgumu wa kisisa ili kuweza kurejea katika mapatano hayo.

Kwa kutilia maanani uvunjaji ahadi wa Marekani na nchi za Ulaya kuhusiana na mapatano ya JCPOA hivi sasa Iran inataka kupewa dhamana ya kutosha kutoka pande hizo kabla ya kuhuishwa mapatano hayo. Kwa kuzingatia uzoefu wa Marekani kujitoa JCPOA, Iran ina haki ya kudai kudhaminiwa baadhi ya mambo ili isitumbukie tena katika matatizo yaliyojitokeza huko nyuma.

Mazungumzo ya JCPOA mjini Vienna Austria

Katika uwanja huo, Mahmoud Waidhi, Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, Iran haitakubali kuwa mwanchama wa mapatano ambayo yanailazimisha kutekeleza majukumu yake bila ya wengine kulazimishwa kufanya hivyo, na kwa msingi huo kuna ulazima wa Marekani kutoa dhamana ya kutojitoa tena katika mapatano ya JCPOA.

Hakuna tofauti yoyote iliyoonekana hadi sasa kuhusu siasa za serikali ya Biden na Donald Trump kuhusu suala zima la JCPOA na kungalipo na shaka kubwa kuhusiana na nia ya Marekani ya kuheshimu na kutekeleza ahadi zake za mapatano hayo. Masuala yote kuhusu udharura wa pande zilizotia saini mapatano ya JCPOA kuheshimu na kutekeleza ahadi zao yamejadiliwa na sasa imebakia tu hatua ya Marekani na nchi tatu za Ulaya kuchukua maamuzi magumu ya kisiasa kuhusiana na suala hilo.

Mbali na kutaka kupewa dhamana kutoka kwa Marekani, Iran inataka pia ihakikishe kivitendo kwamba nchi hiyo imeiondolea vikwazo vya upande mmoja. Kwa mtazamo wa Iran, ni jambo la dharura kuhakikishiwa na Marekani kwamba imeondolewa vikwazo, kwa maana kwamba nchi hiyo ya Magharibi inapasa kutekeleza ahadi zake za JCPOA na kuondoa kivitendo vikwazo ilivyoiwekea Iran na kisha serikali ya Tehran ihakikishe kuwa kweli vikwazo hivyo vimeondolewa, na hapo ndipo itaanza tena kutekeleza ahadi zake za mapatano hayo.

Mahmoud Waidhi, Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Misimamo na matamshi yanayotolewa hivi sasa na watawala wa Marekani kuhusiana na suala zima la JCPOA yameongeza wasi wasi wa Iran kuhusu masuala hayo mawili muhimu yaani kutolewa dhamana na kuhakikisha kuondolewa vikwazo. Ni wazi kuwa kama haitadhaminiwa maslahi yake ya kitaifa, Iran haitatia saini mapatano ya kuhuishwa JCPOA.

Katika uwanja huo, Maria Zakharova, Msmaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema kwamba kufikia sasa Marekani haijachukua hatua yoyote ya kurekebisha siasa za serikali iliyotangulia kuhusu Iran wala kuhusu suala la kuhuishwa mapatano ya JCPOA.

Tags