Bunge la Iran laanza kuchunguza sifa za mawaziri waliopendekezwa na Rais Raisi
(last modified Sat, 14 Aug 2021 08:08:23 GMT )
Aug 14, 2021 08:08 UTC
  • Bunge la Iran laanza kuchunguza sifa za mawaziri waliopendekezwa na Rais Raisi

Msemaji wa kamati ya uongozi ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amesema, bunge hilo linaanza mchakato wa kuchunguza sifa za mawaziri wa serikali mpya waliopendekezwa na Rais Ebrahim Raisi.

Sayyid Nezamuddin Musavi amesema hayo pembeni ya kikao cha leo cha bunge na kueleza kwamba, katika barua aliyoandika Jumatano iliyopita, Seyyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliwasilisha bungeni orodha ya mawaziri aliowapendekeza kuhudumu katika serikali yake.

Musavi ameongeza kuwa, barua hiyo ya Rais Raisi imewasilishwa rasmi leo kwenye kikao cha wazi cha bunge.

Msemaji wa kamati ya uongozi ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amekumbusha kuwa, hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la katiba ambayo imelikabidhi bunge mamlaka ya kuchunguza sifa za mawaziri wanaopendekezwa na kuwapitisha kwa kuwapigia kura za kuwa na imani nao.

Sayyid Nezamuddin Musavi

Amesema, baada ya kikao cha leo cha Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, kamati za utaalamu za bunge hilo zitaanza kufanya vikao vya kujadili na kuchunguza sifa za mawaziri waliopendekezwa.

Sayyid Nezamuddin Musavi amefafanua kuwa, kila waziri aliyependekezwa atafika mbele ya kamati 14 za kitaalamu na kamati mbili maalum ili kuwasilisha programu zake na hadi ifikapo mwishoni mwa wiki, vitakuwa vimeshafanywa vikao 270 vya majadiliano katika kamati hizo na mawaziri 19 waliopendekezwa kuunda serikali mpya.

Kwa mujibu wa msemaji wa kamati ya uongozi ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, kuanzia Jumamosi ya wiki ijayo, na kwa muda wa siku nne, kazi ya kujadili sifa za mawaziri waliopendekezwa itafanyika katika kikao cha wazi cha bunge, ambapo wabunge watatoa uamuzi wao rasmi wa kumkubali au kumkataa kila waziri aliyependekezwa.../