Sep 29, 2024 06:10 UTC
  • Ghalibaf: Sayyid Hassan Nasrullahh ameuawa shahidi katika njia ya ukombozi wa Quds

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameuawa shahidi katika njia takatifu ya kuupigania Uislamu na ukombozi wa Quds.

Mohammad-Bagher Ghalibaf amesema hayo katika ujumbe maalumu wa pongezi na tanzia kufuatia kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah na kusema kuwa, shahid Nasrullah alikuwa kimbilio na wasio na pa kukimbilia, alikuwa ni Sayyid wa Muqawama, kipenzi ya wanyonge duniani, kiongozi anayejitolea muhanga, mpiganaji jihadi asiyechoka na Katibu Mkuu mwaminifu na ameuliwa shahidi na genge la waovu mno la watenda jinai la Wazayuni.

Spika wa Bunge la Iran ameongeza kuwa, waungaji mkono wa Wazayuni wakiongozwa na Marekani wamewathibitishia walimwengu wote jinsi walivyo na kiu isiyokatika ya kufyonza damu za wanawake, watoto wadogo wasio na hatia wakimbizi na watu wasio na pa kukimbilia.

Ameongeza kuwa, Sayyid Hassan Nasrullah amepata mafanikio makubwa katika umri wake uliojaa baraka kwenye njia ya kupambana na adui Mzayuni na kulidhaminia usalama taifa la Lebanon kama ambavyo pia amefanikiwa kufungua njia ya ukombozi wa Quds kwa hikma na busara kubwa.

Jana tarehe 28 Septemba 2024, Hizbullah ya Lebanon ilitoa taarifa ya kuthibitisha kuuawa shahidi, Katibu Mkuu wake, Sayyid Hassan Nasrullah katika mashambulizi ya kikatili ya Wazayuni ya Ijumaa usiku.    

Tags