May 28, 2025 02:05 UTC
  • Jumatano tarehe 28 Mei 2025

Leo ni Jumatano tarehe Mosi Mfunguo Tatu Dhul-Hijja 1446 Hijria mwafaka na tarehe 28 Mei 2025.

Siku kama ya leo miaka 1444 iliyopita Binti wa Mtume Muhammad (saw) Fatima al Zahra (as) alifunga ndoa na Imam Ali bin Abi Twalib (as) Bibi Fatima alikuwa mwanamke mwema aliyejipamba kwa sifa zote nzuri ambaye alichumbiwa na shakhsia wakubwa na watu mashuhuri wa zama hizo.

Hata hivyo Mtume (saw) alikuwa akiwaambia wachumbiaji hao kwamba suala la kuolewa Fatima liko mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Hatimaye Imam Ali bin Abi Twalib alikwenda kwa Mtume na kumchumbia Bibi Fatima na baada ya kushauriana na bintiye, Mtume alikubaliana na ombi la Ali na kuwafungisha ndoa. Baada ya kufunga ndoa, watukufu hao wawili waliishi maisha ya watu wa kawaida lakini yaliyojaa upendo, masuala ya kiroho na maadili ya Kiislamu. Watukufu hao wawili waliipa jamii ya mwanaadamu watu adhimu na kamili kama Imam Hassan, Imam Hussein na Bibi Zainab (as).

Ali na Fatima (as) walikuwa kigezo bora cha mwanaadamu kamili.*

Miaka 860 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Ibn Abi al-Hadid alimu na mwanahistoria mkubwa wa Kiislamu.

Abu Hamid Abdul-Hamid bin Muhammad Madayini maarufu kwa jina la Ibn Abil-Hadid Mu'tazili, ni mmoja wa wanazuoni wakubwa wa Muu'tazila, fakihi, mshairi, mwanafalsafa na mwandishi.

Kitabu chake cha Sharh ya Nahajul-Balagha ambacho kimempatia umashuhuri zaidi kinadhihirisha mapenzi yake makubwa kwa Amirul-Muminina Ali bin Abi Twalib (as) na familia ya Mtume (saw).

Siku kama ya leo miaka 173 iliyopita, alifariki dunia Eugène Burnouf, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati wa Ufaransa. Burnouf alizaliwa Paris mwaka 1801 na kuhitimu somo la sheria. Hata hivyo hamu yake kubwa ya kusomea lugha na fasihi sambamba na kuvutiwa na masuala ya Mashariki ya Kati, vilimfanya ajifunze lugha za Sanskrit na Iran ya kale. Eugène Burnouf pia alijifunza utamaduni wa nchi za Iran na India. Miongoni mwa kazi zilizozifanya msomi huyo ni pamoja na kufasiri sehemu za kitabu cha Avesta. Vitabu vya ‘Dondoo za Yasna’ ‘Historia ya dini ya Mabudha’ na ‘Babr Bayan’ ni miongoni mwa vitabu vya Eugène Burnouf.

Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, sawa na tarehe 28 Mei 1940, Ubelgiji ambayo ilitangaza kutoegemea upande wowote mwanzoni mwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, ilitekwa na majeshi ya Kinazi ya Ujerumani.

Majeshi ya Ubelgiji ambayo yalikuwa yakipata usaidizi wa Uingereza, yalisimamisha vita kutokana na amri ya Mfalme Leopold wa Tatu, licha ya kusimama kidete kwa muda wa siku 18 dhidi ya majeshi ya Kinazi ya Ujerumani.

Hatua hiyo ya Mfalme Leopold, iliwakasirisha mno wananchi wa Ubelgiji na kuandaa mazingira ya kuondolewa kwake madarakani hapo mwaka 1951. 

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, sawa na tarehe 28 Mei 1964, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu iliafikiana na fikra ya kubuniwa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO ambapo mwanzoni ilizijumuisha harakati nane za mapambano pamoja na idadi kubwa ya taasisi za kielimu, kijamii, kitiba, kiutamaduni na kifedha.

Mwaka mmoja baadaye tawi la kijeshi la Fat'h ambalo lilikuwa na wanachama 10,000 likaanzisha shughuli za kupigania ukombozi wa Palestina. Mwaka 1974 PLO ilikubaliwa kuwa manachama mtazamaji katika Umoja wa Mataifa ambapo kufikia mwaka 1982 ilikuwa imeanzisha uhusiano rasmi na zaidi ya nchi 100 za dunia.

Taratibu PLO ilianza kupoteza muelekeo wake wa kupambana kijeshi na utawala ghasibu wa Israel ambapo kufikia mwaka 1993, ikiongozwa na Yassir Arafat, ilikubali kuutambua rasmi utawala huo kwa kutia saini mapatano ya Oslo hapo mwaka 1993.   

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita sawa na tarehe 28 Mei 1991, utawala wa kikomunisti wa Mengistu Haile Mariam ulisambaratika nchini Ethiopia na kupelekea mtawala huyo dikteta kukimbia nchi.

Ethiopia ni moja ya nchi kongwe zaidi barani Afrika na wakati mmoja ilikuwa sehemu ya utawala wa kifalme wa Misri ya kale. Tokea karne ya 16 Milaadia wakoloni wa Ureno, Uingereza na Italia walifanya juhudi kubwa za kuikoloni nchi hiyo kwa lengo la kupora utajiri wake lakini bila mafanikio makubwa.

Italia iliishambulia Ethiopia mara mbili, shambulio la kwanza likifanyika mwaka 1896 ambapo ilishindwa kufikia malengo yake na la pili likafanyika mwaka 1936 ambapo iliikalia Ethiopia kwa muda wa miaka mitano. Mfalme wa mwisho kuitawala Ethiopia alikuwa Haile Selassie ambaye aliitawala nchi hiyo tokea mwaka 1930 hadi 1974 na kisha akapinduliwa na watawala wa kikomunisti, ambao nao baadaye walikabiliwa na upinzani mkubwa wa ndani kutokana na majanga ya njaa na matatizo mengine yaliyotokana na utawala mbaya.   

Mengistu Haile Mariam

Na siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 28 Mei 1998, kwa mara ya kwanza Pakistan ilifanya majaribio matano ya makombora ya nyuklia.

Majaribio hayo yalifanyika zikiwa zimepita wiki mbili tu tangu hasimu wake, yaani India, ifanye majaribio ya kombora la nyuklia. Baada ya hapo nchi hizo mbili zimekuwa zikifanya kwa zamu majaribio yao ya makombora ya nyuklia.

Majaribio ya nyuklia ya Pakistan, kinyume na yale yanayofanywa na India,  yamekuwa yakizikasirisha mno nchi za Magharibi za Marekani na Ulaya, na kufikia hatua ya kuiwekea nchi hiyo vikwazo vya kiuchumi.