Kamanda Rashid: Maadui wasiujaribu uwezo wa IRGC na jeshi la Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i76654-kamanda_rashid_maadui_wasiujaribu_uwezo_wa_irgc_na_jeshi_la_iran
Kamanda wa Makao Makuu ya Kamandi ya Kijeshi ya Khatamul Anbiya ya Iran amewatahadharisha maadui wa Jamhuri ya Kiislamu dhidi ya kuujaribu uwezo wa jeshi la nchi hii na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 07, 2021 23:14 UTC
  • Kamanda Rashid: Maadui wasiujaribu uwezo wa IRGC na jeshi la Iran

Kamanda wa Makao Makuu ya Kamandi ya Kijeshi ya Khatamul Anbiya ya Iran amewatahadharisha maadui wa Jamhuri ya Kiislamu dhidi ya kuujaribu uwezo wa jeshi la nchi hii na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

Meja Jenerali Gholam Ali Rashid alitoa indhari hiyo jana Jumapili wakati wa kuanza mazoezi ya kijeshi yaliyopewa jina la Dhulfiqar-1400 yanayofanyika huko kusini mashariki mwa nchi.

Amesema vikosi vya majeshi ya Iran daima vipo tayari kwa ajili ya operesheni zozote za kistarajia za kujibu chokochoko za maadui, na kuimarisha usalama, uthabiti na mamlaka ya kujitawala taifa hili, mkabala wa miungano ya maadui (hususan muungano wa Marekani na Wazayuni).

Kamanda Rashid ameeleza bayana kuwa,  vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vitatoa jibu mwafaka kwa uchokozi wowote wa madola ya kiistikbari na wavamizi kwa kiwango chochote.

Kuanza luteka ya baharini, angani na nchi kavu ya 'Dhulfiqar-1400'

Luteka hiyo ya kijeshi ilianza jana Jumapili katika eneo la Makran, kusini mashariki mwa Iran, ikijumuisha vikosi vya nchi kavu, ndege zisizo na rubani (droni), manowari, na ndege za kivita.

Msemaji wa maneva hayo ya kijeshi ya Dhulfiqar-1400, Admeri Mahmoud Mousavi amesema, ujumbe wa mazoezi hayo ya kijeshi ni amani na urafiki kwa ajili ya nchi jirani na kanda ya magharibi mwa Asia na tahadhari kwa majeshi ya nchi ajinabi ambazo zinafanya jitihada za kuchafua amani na usalama wa eneo nyeti na la kistratijia la Ghuba ya Uajemi.

Admeri Mousavi ameongeza kuwa, usalama utapatikana katika Asia Magharibi kupitia umoja wa nchi za eneo hili, na kwa nchi zenyewe kutegemea uwezo wao badala ya kuzitegemea nchi ajinabi.