Momeni :Iran inashika rekodi ya dunia ya kukamata dawa za kulevya
-
Brigedia Jenerali Eskandar Momeni
Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Mihadarati nchini Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inashika rekodi ya dunia ya kukamata dawa za kulevya.
Brigedia Jenerali Eskandar Momeni leo Jumapili ameeleza kuwa, mihadarati ni miongoni mwa maafa makubwa ya binadamu na chanzo cha masaibu mengi na kuongeza kuwa: Katika kipindi cha miaka 40 iliyopita tumepata mafanikio makubwa katika kukabiliana na magendo ya dawa za kulevya na Umoja wa Mataifa umetangaza rasmi kuwa asilimia 90 ya mihadarati aina tiryak, asilima 70 ya madawa ya kulevya aina ya morphine, na asilimia 20 ya madawa yote ya kulevya aina ya heroine yameyokamatwa na Iran.
Brigedia Jenerali Momeni amesisitiza kuwa, zaidi ya askari usalama elfu 12 wa Iran ama wamejeruhiwa au kuuliwa shahidi wakipambana na magenge ya dawa za kulevya na kuongeza kuwa: Mwaka uliopita karibu tani 1200 za mihadarati zilikamatwa, kiwango ambacho ndicho cha juu zaidi duniani.
Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Mihadarati nchini Iran amesema kuwa kuwepo kwa Wamarekani nchini Afghanistan ndiyo sababu ya kuongezeka uzalishaji wa mihadarati na amekumbusha kuwa: Mwaka 2000, uzalishaji wa jumla wa dawa za kulevya nchini Afghanistan ulikuwa takriban tani 200, na mwaka 2018 kiwango hicho kiliongezeka na kifikia tani 9,000; kwa maana kwamba kilimo na uzalisha wa dawa za kulevya uliongezeka mara hamsini nchini Afghanistan; jambo ambalo limeongeza maradufu haja ya kuzidishwa juhudi za kupambana na janga hilo.