Umoja wa Mataifa waipongeza Iran kwa kuwapa huduma wakimbizi
Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNCHR) ameipongeza Iran kwa ukarimu wake mkubwa katika kuwapa huduma wakimbizi hasa wale waliodhulumiwa kutoka nchi jirani ya Afghanistan.
Akizungumza Jumapili, Filippo Grandi ameashiria muamala mwema na wa kibinadamu wa watu wa Iran kwa wakimbizi na kuongeza kuwa Umoja wa Mataifa unajitahidi kuhakikisha amani inarejea Afghanistan ili kuandaa mazingira ya wakimbizi kurejea.
Grandi ameyasema hayo mjini Tehran wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran Hussein Zulfaqari.
Hivi karibuni pia mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani nchini Iran Dakta Jafar Hussain naye pia ameipongeza Iran kwa kutoa huduma nzuri za afya kwa wakimbizi wa Afghanistan ambapo ametoa mfano wa huduma za chanjo ya COVID-19 walizopata wakimbizi hao kote Iran.
Amesema kuna wakimbizi baina ya milioni tatu hadi milioni nne wa Kiafghani nchini Iran ambapo amesema Iran iliwapatia chanjo wakimbizi hao bila ubaguzi. Aidha wakimbizi Waafghani nchini Iran wanapata huduma za elimu sawa na watoto Wairani.
Mwaka 2015, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei, alisema hivi kuhusu haki ya kupata elimu watoto wakimbizi kutoka Afghanistan hata wale ambao wako nchini kinyume cha sheria: "Mtoto Muafghani, hata yule ambaye yuko Iran kinyume cha sheria na bila nyaraka zozote, hapaswi kunyimwa fursa ya kujiendeleza kimasomo na wote wanapaswa kusajiliwa katika shule za Iran."
Agizo hilo la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu ulazima wa watoto wote Waafghani nchini Iran kupata masomo katika shule za serikali ni kati ya sera bora zaidi za kuwahudumia wakimbizi na sera kama hiyo ni ya aina yake na ya kipekee duniani.