Abu Turabi Fard: Marekani na Israel zinavuruga amani Asia Magharibi
-
Sayyid Muhammad Hassan Abu Turabi Fard
Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran amesema kuwa, katika zama hizi za giza ambapo siasa za Marekani na mamluki wake zinachochea ukosefu wa usalama na machafuko katika eneo la Magharibi mwa Asia na dunia, mfumo wa Kiislamu wa Iran umeweza kuboresha pakubwa kiwango cha usalama katika eneo hilo.
Hujatul-Islam Wal-Muslimin Sayyid Muhammad Hassan Abu Turabi Fard ameyasema hayo katika hotuba za Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran iliyohudhuriwa na maelfu ya waumini.
Katika hotuba ya kwanza ya Swala ya Ijumaa Sayyid Abu Turabi-Fard ameashiria dikrii ya Imam Ali bin Abi Twalib kwa aliyekuwa gavana wake nchini Misri, Malik al Ashtari na watawala wote wa historia kuhusu sifa muhimu za utawala bora na sahihi na kusisitiza kuwa, mfumo wa kudhamini fedha na kipato na mfumo wa ulinzi ni nyenzo mbili muhimu za utawala madhubuti. Amesisitiza kuwa, bila ya kuwa mfumo madhubuti na wa kuaminika wa fedha na kudhamini amani haiwezekani kutayarisha njia sahihi ya jamii kuelekea kwenye saada na ufanisi.
Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran amekumbusha nafasi na mchango mkubwa wa Shahidi Luteni Jenerali Qasem Soleimani katika kuimarisha amani kwenye eneo la Asia Masharibi na ulimwenguni na kusema kuwa: "Shahidi Soleimani na wenzake waliwadhaminia amani na usalama wananchi wa Iran, eneo la Asia Magharibi na hata Ulaya ya dunia kutokana na mapambano yao dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh.
Sayyid Abu Turabi-Fard amesema: "Katika hali ambayo Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel wanaendelea kuvuruga amani na utulivu katika eneo la Asia Magharibi, Mfumo wa Kiislamu wa Iran umeweza kuongeza kwa kiasi kikubwa kiwango cha usalama katika eneo hili na kufungua njia ya kuimarisha amani na uwezo wa kujilinda, sio tu kwa Iran bali pia kwa ulimwengu wa Kiislamu.