Shauku maradufu ya Azerbaijan ya kupanua ushirikiano na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i78742-shauku_maradufu_ya_azerbaijan_ya_kupanua_ushirikiano_na_iran
Viongozi wa Iran na Jamhuri ya Azerbaijan wakiwa na lengo la kupanua uhusiano wa pande mbili na kustawisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara wamo mbioni kupiga hatua kubwa katika uwanja huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 02, 2022 09:23 UTC
  • Shauku maradufu ya Azerbaijan ya kupanua ushirikiano na Iran

Viongozi wa Iran na Jamhuri ya Azerbaijan wakiwa na lengo la kupanua uhusiano wa pande mbili na kustawisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara wamo mbioni kupiga hatua kubwa katika uwanja huo.

Baada ya Marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jamhuri ya Azerbaijan kukutana na kufanya mazungumzo pambizoni mwa mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi (ECO) na mkutano wa wakuu wa mataifa ya Ukanda wa Bahari ya Caspian huko Ashgabat Turkemanistan na vilevile safari ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran huko Azerbaijan, kumezidi kuimarishwa nyanja za ushirikiano wa pande mbili na kieneo baina ya Tehran na Baku.

Kuhusiana na hilo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Azerbaijan imetangaza katika taarifa yake maalumu kwamba: Mazungumzo ya Marais Ilham Alyev na Ibrahim Raeisi mwishoni mwa Novemba mwaka jana, ni jambo ambalo limeandaa uwanja na kuleta msukumo maradufu kwa viongozi wa Baku kwa minajili ya kupanua ushirikiano wao na Tehran kadiri iwezekanavyo.

Sehemu moja ya taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Azerbaijan imeeleza: Katika mwaka uliomalizika juzi wa 2021 kumefanywa juhudi za kuhakikisha kwamba, kunadumishwa uhusiano wa kirafiki na wa ujirani mwema na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kiwango cha juu kabisa.

Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Azerbaijan imetolewa katika hali ambayo, Ilham Aliyev Rais wa Jamhuri ya Azebajan nchi pekee ya Kiislamu kaskazini mwa Aras alisema hivi karibuni kwamba: Baku imetumia njia zote za kidiplomasia kwa ajili ya kuondoa suutafahamu zilizojitokeza baina yake na Tehran; kwani hakuna wakati ambao siyo huko nyuma au hivi sasa ambapo Jamhuri ya Azerbaijan ilitamani kuona uhusiano wake na Tehran unafifia na kudorora.

Ilham Aliyev, Rais wa Azerbaijan katika moja ya safari zake nchini Iran akiwa katika mazungumzo na Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

 

Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Azerbaijan na matamshi ya hivi karibuni ya Rais wa nchi hiyo ni kielelezo bayana cha hamu na shauku ya hali ya juu waliyonayo viongozi wa Baku ya kudumisha ushirikiano wao na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ni katika hali ambayo, viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nao wamesisitiza mara chungu nzima kwamba, hawana mpaka katika uwanja wa ushirikiano na mataifa jirani na wana raghba na shauku ya dawamu ya kufuatilia ushirikiano wa pande mbili katika kiwango cha juu.

Ni jambo lisilo na shaka kwamba, katika miaka ya hivi karibuni uingiliaji wa wanasiasa ajinabi katika masuala ya ndani ya Azerbaijan umeandaa uwanja wa kuleta kuharibifu kwa muda katika uhusiano wa pande mbili hizi jirani. Miongoni mwao tunaweza kuashiria hapa uingiliaji wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika masuala ya ndani ya serikali ya Rais Ilham Aliyev.

Hapana shaka kuwa, endapo mwenendo wa Israel wa kuingilia masuala ya ndani ya Azerbaijan utaendelea, uhusiano na ushirikiano wenye wigo mpana na usio na mipaka wa nchi mbili za Kiislamu na jirani za Iran na Azerbaijan utakumbwa na hali tete.

 

Kimsingi tunapaswa kusema kuwa, hatua ya viongozi wa Azerbaijan ya kuuruhusu utawala ghasibu wa Israel unaoikalia kwa mabavu Baytul-Muqaddas kuwa na maamuzi kuhusiana na uhusiano wa Tehran na Baku kutauandalia uwanja mwafaka utawala huo wa kibaguzi wa kuweza kupanda na kustawisha mbegu ya chuki na hasama baina ya nchi mbili hizi jirani za Kiislamu.

Hii ni katika hali ambayo, daima Iran na Azerbaijan zimekuwa zikipanga mikakati ya kupanua ushirikiano wa pande mbili na wa kieneo na kufanya hima na idili kwa shabaha ya kuimarisha ushirikiano sambamba na kuondoa mipaka na vizingiti vyote vilivyoko katika njia ya kufikiwa hilo.

Hata hivyo katika miezi ya mwishoni mwa mwaka uliomalizika wa 2021, viongozi wa Azerbaijan hususan Rais Ilham Aliyev alihamasishwa na kuelekea upande wa mizozo na kutoa tuhuma zisizo na kichwa wala miguu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana wanafikra na wakomavu katika uga wa kisiasa wakajitokeza mara kadhaa na kuitahadharisha serikali ya Ilham Aliyev.

Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran (kulia) na Azerbaijan

 

Kwa mfano tunaweza kuashiria indhari na matamshi ya Ilgar Ibrahimoglu, Mkuu wa Kituo cha Kuunga Mkono Dhamira na Uhuru wa Kidini (DEVAMM) ambaye pia ni mwanafikra na mwananadharia mtajika wa masuala ya kisiasa na kidini kaskazini mwa Aras ambaye anaamini kuwa: Jamhuri ya Azerbaijan haipasi kugeuzwa na kufanywa uwanja wa mivutano ya madola shindani na watu ambao wanataka kumaliziana mahesabu yao. Hawapaswi kuzileta hitilafu zao hizo katika ardhi ya Azerbaijan

Ni wazi kwamba, matamshi ya mweledi na msomi huyo mwanasiasa wa Azerbaijan yanaonyesha kuwa, utawala wa Israel unaoikalia kwa mabavu Baytul-Muqaddas una satua na ushawishi nchini Azerbaijan na umeigeuza ardhi ya nchi hiyo ya Kiislamu na kuifanya kuwa uwanja wa kumaliziana mahesabu na Tehran.

Ala kulli haal, tunaweza kusema katika natija jumla kuhusiana na uhusiano wa Tehran na Baku kwamba: Kupatiwa ufumbuzi wa matatizo ya Azerbaijan na Armenia kutaandaliwa uwanja zaidi wa ushirikiano wa pande mbili wa Tehran na Baku pamoja na ushirikiano wa kieneo wa nchi mbili hizi jirani. Inaonekana kuwa, kutekelezwa makubaliano yenye vipengee 10 vya hati ya makubaliano ya amani ya Karabakh kutaandaa uwanja mwafaka zaidi wa kuweko mabadilishano ya kibiashara na ushirikiano wa kiuchumi wa Iran na mataifa ya Azerbaijan na Armenia.