Iran: Wakazakhstan wanaweza kutatua matatizo yao bila uingiliaji wa maajinabi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i78910-iran_wakazakhstan_wanaweza_kutatua_matatizo_yao_bila_uingiliaji_wa_maajinabi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema wananchi wa Kazakhstan wana uwezo wa kuupatia ufumbuzi mgogoro uliopo, pasi na kutegemea uingiliaji wa madola ajinabi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 07, 2022 00:03 UTC
  • Iran: Wakazakhstan wanaweza kutatua matatizo yao bila uingiliaji wa maajinabi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema wananchi wa Kazakhstan wana uwezo wa kuupatia ufumbuzi mgogoro uliopo, pasi na kutegemea uingiliaji wa madola ajinabi.

Saeed Khatibzadeh alisema hayo jana Alkhamisi, akitoa radiamali yake kwa hali ya mchafukoge inayoendelea kushuhudiwa katika nchi hiyo ya Asia ya Kati. 

Huku akisisitiza kuwa anatumai kuwa hali ya utulivu itarejea katika nchi hiyo haraka iwezekanavyo, Khatibzadeh amesema kuwa, "Serikali na wananchi wenye busara wa nchi jirani na rafiki ya Kazakhstan wanaweza kutatua matatizo yao bila uingiliaji wa maajinabi."

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amebainisha kuwa, uthabiti na usalama wa Kazakhstan una umuhimu mkubwa sana kwa Jamhuri ya Kiislamu; na kwamba Wakazaki hawapaswi kuruhusu uingiliaji wa masuala ya ndani ya nchi yao na mawakala wa nchi za kigeni.

Hali ya mshikemshike Kazakhstan

Kwa siku kadhaa sasa, wananchi wa Kazakhstan wamekuwa wakifanya maandamano ya kulalamikia hatua ya serikali ya kupandisha bei ya mafuta. Makumi ya watu wakiwemo maafisa usalama wameuawa kwenye maandamano hayo yaliyoibuliwa na madereva Jumapili iliyopita katika mji wa Zhanaozen katika eneo la Mangystau.

Ifahamike kuwa, nchi hiyo ya katikati mwa bara Asia ni miongoni mwa nchi zenye utajiri mkubwa wa mafuta duniani.