May 29, 2016 04:13 UTC
  • Iran yafadhili mashindano ya Qur'ani katika Televisheni ya Uganda

Kitengo cha Utamaduni cha Iran nchini Uganda kimefadhili mashindano ya Qur'ani Tukufu katika Televisheni ya Taifa ya nchi hiyo, UBC.

Mkuu wa Kitengo cha Utamaduni cha Iran katika mji mkuu wa Uganda, Kampala, Ali Bakhtiari amesema katika mahojiano na Shirika la Habari la Kimataifa la Qur'ani Tukufu IQNA kwamba, harakati za Qur'ani za idara hiyo nchini Uganda zimejikita katika masuala ya kuelimisha na kuandaa mashindano ya Qur'ani.

Ameongeza kuwa, aghalabu ya harakati za Qur'ani za kitengo hicho katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ni kuunga mkono mashindano ya Qur'ani katika viwango mbalimbali vya kitaifa, vyuo vikuu na shule.

Bakhtiari ameongeza kuwa, Idara ya Utamaduni ya Iran nchini Uganda mbali na kushiriki katika harakati za Qur'ani katika vituo vya kidini na madrasa za Qur'ani, kila mwaka huandaa mashindano ya Qur'ani katika kiwango cha kitaifa kwa ushirikiano na Televisheni ya Taifa ya Uganda, UBC, mashindano ambayo yatafanyika pia mwaka huu.

Ameongeza kuwa, mashindano hayo yatarushwa hewani moja kwa moja katika kanali mbili za televisheni ya Uganda UBC. Bw. Bakhtiari amesema mashindano hayo ya Qur'ani katika televisheni yatahudhuriwa pia na qarii wa kimataifa pamoja na kundi la wasomaji qasida kutoka Iran.

Aidha amesema Kitengo cha Utamaduni cha Iran kinashirikiana na televisehni ya Kiislamu ya Salam TV katika kurusha hewani vipindi vya tafsiri na maarifa ya Qur'ani Tukufu.

Aidha amesema idara hiyo ya utamaduni inashirikiana na taasisi mbali mbali za Kiislamu nchini Uganda hasa katika masuala harakati za Qur'ani, kuleta umoja baina ya Waislamu, amani duniani, vijana na wanawake.

Tags