Mkurugenzi mkuu wa wakala wa IAEA kuitembelea Iran kesho
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) anatazamiwa kuitembelea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kesho Jumamosi kwa ziara rasmi ya kikazi.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Rafel Grossi anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Muhammad Eslami, Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran (AEOI) ambapo watachunguza hali ya ushirikiano wa kiufundi wa pande mbili.
Aidha anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na maafisa wengine wa ngazi za juu wa Iran katika safari ambayo ina umuhimu katika kuendeleza ushirikiano wa pande mbili na pia kufuatilia kadhia mbalimbali za pande mbili katika anga iliyo bora.
Safari ya Grossi hapa jijini Tehran inatazamiwa kuchunguza na kutafutia ufumbuzi mvutano uliopo kuhusu shughuli za nyuklia za Iran, na masuala yanayohusiana na mkakati wa kulinda makubaliano kati ya IAEA na AEOI.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitilia mkazo umuhimu wa kufanywa mambo kiufundi na kiutaalamu, kutopendelea upande wowote Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na kutokubali wakala huo kushinikizwa kisiasa na madola ya kigeni.
Haya yanajiri huku awamu ya nane ya mazungumzo ya Vienna kwa ajili ya kuiondolea Iran vikwazo vya kidhulma ilivyowekewa na Marekani mwaka 2018, ikiendelea huko Austria.