Iran na EU zajadili masuala yaliyosalia katika mazungumzo ya Vienna
Kiongozi wa timu ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia ya Vienna, Ali Baqeri Kani amekutana na kufanya mazungumzo hapa mjini Tehran na Enrique Mora, mratibu wa mazungumzo ya Vienna, ambapo wamejadili hatua zilizopigwa na masuala yaliyosalia katika mazungumzo hayo yanayofanyika huko Austria.
Ali Baqeri Kani amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejitolea kwa dhati na ina izma ya kweli ya kuona mazungumzo hayo yanafikia tamati.
Baqeri Kani ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amebainisha kuwa, iwapo Marekani itatazama mambo kwa uhalisia wake, basi makubaliano yanaweza kufikiwa.
Kwa upande wake, Enrique Mora, mratibu wa mazungumzo ya Vienna ambaye pia ni Naibu Mkuu wa Sera za Nje za Umoja wa Ulaya amewasilisha ripoti kuhusu mashauriano ya hivi karibuni ya pande zingine za mapatano ya JCPOA.

Afisa huyo wa EU na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran anayehusika na masuala ya kisiasa wanatazamiwa kuendelea kushauriana katika siku zijazo kuhusu masuala yaliyosalia katika mazungumzo ya Vienna.
Duru ya nane ya mazungumzo ya Vienna, yanayofanyika kwa lengo la kuiondolea Iran vikwazo vya kidhalimu na kinyume cha sheria ambayo ilianza Februari 8 mwaka huu katika mji mkuu huo wa Austria ilisitishwa kwa mara nyingine tena tarehe 11 mwezi huu.