Apr 03, 2022 03:22 UTC
  • Iran yawanyooshea mkono wa kheri Waislamu duniani kwa kuwadia Ramadhani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewapongeza na kuwatakia Waislamu wote duniani kheri na baraka kwa mnasaba wa kuwadia mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter jana Jumamosi kwa lugha ya Kiarabu, Hossein Amir-Abdollahian ameandika: Pongezi kwa Umma wote wa Kiislamu duniani, kwa kuwadia mwezi mtukufu wa Ramadhani, mwezi wa huruma.

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kwa kuandika: Tunamuomba Allah Atupe sote kheri tele, amani na baraka.

Baadhi ya mataifa ya Kiislamu kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Iraq na Oman yametangaza kuwa, leo Jumapili ndiyo siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei ilitangaza Ijumaa usiku kwamba leo Jumapili ndio mwezi Mosi wa Ramadhani.

Hata hivyo baadhi ya nchi kama Indonesia, Uturuki, Mauritania, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Qatar, Kuwait, Palestina, na Misri zilianza funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani jana Jumamosi.

Radio Tehran, Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inawaombea na kuwatakia Waislamu wote duniani kheri na baraka za mwezi huo mtukufu ambao ni hiba, atia na zawadi kubwa sana inayotoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waja wake anaowapenda.

Tags