Iran na Iraq zatoa mwito wa kutekelezwa makubaliano ya pande mbili
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i82298-iran_na_iraq_zatoa_mwito_wa_kutekelezwa_makubaliano_ya_pande_mbili
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hossein Amir-Abdollahian na mwenzake wa Iraq, Fuad Hossein wamesisitizia haja ya kuharakishwa mchakato wa kutekelezwa makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa huko nyuma baina ya nchi mbili hizi jirani za Kiislamu.
(last modified 2026-01-14T11:42:18+00:00 )
Apr 09, 2022 02:31 UTC
  • Iran na Iraq zatoa mwito wa kutekelezwa makubaliano ya pande mbili

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hossein Amir-Abdollahian na mwenzake wa Iraq, Fuad Hossein wamesisitizia haja ya kuharakishwa mchakato wa kutekelezwa makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa huko nyuma baina ya nchi mbili hizi jirani za Kiislamu.

Hossein Amir-Abdollahian na Fuad Hossein walitoa mwito huo jana Ijumaa katika mazungumzo yao ya simu, ambapo walitathmini hatua zilizopigwa kwenye kalibu ya kuimarisha uhusiano wa Tehran na Baghdad katika nyuga tofauti.

Sanjari na kupeana mkono wa mwaka mpya wa Kiirani wa Hijria Shamsia na pongezi kwa kuwadia mwezi mtukufu wa Ramadhani, mawaziri hao wa mambo ya nje wa Iran na Iraq wamejadili masuala yenye maslahi ya pamoja kama vile uhusiano wa pande mbili, masuala ya kieneo na mazungumzo ya Vienna kati ya Iran na kundi la 4+1.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amegusia safari yake ya hivi karibuni mjini Moscow, na mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, ambapo pamoja na mambo mengine, walizungumzia mgogoro wa Ukraine.

Amir-Abdollahian kwa upade wake ameashiria mgogoro huo wa Ukraine na kubainisha kwamba, Tehran inatilia mkazo wajibu wa kutafutwa njia za kisiasa za kuutatua mgogoro huo.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amesisitiza kuwa, kufuatiliwa mizizi ya mgogoro wa sasa ndiko tu kunaweza kuleta amani ya kudumu na uthabiti katika eneo la Eurasia.

Kadhalika Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hossein Amir-Abdollahian amemualika mwenzake wa Iraq, Fuad Hossein kuitembelea Jamhuri ya Kiislamu.