Qalibaf: Kuunda serikali jumuishi ni muhimu ili kuhakikisha usalama wa Afghanistan
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema kuwa kuasisi serikali shirikishi ni jambo lenye umuhimu kwa ajili ya kuhakikisha usalama endelevu nchini Afghanistan.
Afghanistan siku kadhaa za karibuni imekumbwa na milipuko na mashambulizi ya kigaidi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo ukiwemo mji mkuu wa nchi hiyo Kabul, Msikiti wa Mazar- Sharif na huko Qunduz; ambapo mamia ya watu wameuawa na wengine kujeruhiwa. Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limekiri kuhusu na akthari ya milipuko hiyo.
Ijumaa iliyopita duru za habari zilitangaza habari ya kuuawa mamia ya watu katika mlipuko wa bomu uliotokea ndani ya Msikiti wa Waislamu wa madhehebu ya Shia mjini Kabul. Kundi la Taliban ambalo lilishika hatamu za uongozi Afghanistan Agosti 15 mwaka jana, liliadi kuwa litadhamini usalama kote nchini humo.
Muhammad Bager Qalibaf, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amesema katika hotuba yake kabla ya kuanza kikao cha wazi cha Majlisi kwamba: Siku hizi, Marekani inalitumia kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) huko Afghanistan kwa ajili ya kuvuruga usalama katika nchi hiyo lengo kuu likiwa kuibua fitna za kikabila na kidini na kuwatumbukiza wananchi madhulumu wa nchi hiyo katika mgogoro mkubwa.
Qalibaf pia ametoa pongezi na mkono wa baraka kwa Waislamu wote duniani hususan taifa la Iran ya Kiislamu kwa mnasaba wa kuwadia sikkukuu ya Idul Fitr.