Afghanistan yaituhumu Pakistan kwamba imeua watu 400 hospitalini Kabul
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i137424-afghanistan_yaituhumu_pakistan_kwamba_imeua_watu_400_hospitalini_kabul
Afghanistan imelituhumu jeshi la Pakistan kwamba limeua mamia ya watu katika shambulio la anga dhidi ya hospitali moja mjini Kabul.
(last modified 2026-03-17T08:17:49+00:00 )
Mar 17, 2026 08:17 UTC
  • Afghanistan yaituhumu Pakistan kwamba imeua watu 400 hospitalini Kabul

Afghanistan imelituhumu jeshi la Pakistan kwamba limeua mamia ya watu katika shambulio la anga dhidi ya hospitali moja mjini Kabul.

Naibu Msemaji wa Serikali ya Taliban ya Afghanistan, Hamdullah Fitrat amesema watu 400 wameuawa katika shambulio hilo dhidi ya Hospitali ya Omar ya Kutibu Waraibu wa Mihadarati mjini Kabul.

Fitrat amedai kuwa, mbali na watu 400 kupoteza maisha katika hujuma hiyo ya anga ya jeshi la Pakistan, wengine zaidi ya 250 wamejeruhiwa. Amesema sehemu kubwa ya hospitali hiyo yenye vitanda 2,000 vya wagonjwa imeharibiwa kikamilifu.

Hata hivyo, Pakistan imekanusha vikali madai hayo ikisisitiza kuwa, yameibuliwa kwa shabaha ya kupotosha fikra za walio wengi, ikisisitiza kuwa jeshi lake limelenga tu vituo vya kijeshi jijini Kabul na katika mkoa wa Nangahar.

Omid Stanikzai, bawabu wa hospitali hiyo ya kurekebisha tabia amesema walisikia sauti za ndege zikiruka angani, kabla ya kutokea shambulio. Ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, waliouawa na kujeruhiwa katika shambulio hilo ni raia.

Hapo awali, Taliban ilidai kuwa watu wanne wakiwemo watoto wawili wameuawa huku wengine zaidi ya 10 wakijeruhiwa katika makabiliano na jeshi la Pakistan, kusini mashariki mwa Afghanistan.

Pakistan na Afghanistan zimeshuhudia mapigano makali tangu mwishoni mwa mwezi uliopita wa Februari. Pakistan imefanya mashambulizi ya anga katika maeneo kadhaa ya mji mkuu wa Afghanistan, Kabul na pia Kandahar, huku Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan, Mohsin Naqvi akiyaelezea mashambulizi hayo kama "jibu mwafaka" kwa "uchokozi wa wazi wa Taliban." 

Mpaka sasa makumi ya wapiganaji wa Taliban wameuawa katika makabiliano baina ya pande mbili hizo. Pakistan imetangaza kuwa, operesheni hiyo ni jibu kwa hatua zisizo na sababu zilizochukuliwa na Taliban ya Afghanistan katika eneo la mpakani, na kwamba mashambulizi ya anga yangali yanaendelea.