Iran: Tuko tayari kuipa Afghanistan teknolojia ya kupambana na ukame
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i83244-iran_tuko_tayari_kuipa_afghanistan_teknolojia_ya_kupambana_na_ukame
Mjumbe wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya Afghanistan amesema kuwa, Tehran iko tayari kuipa Kabul teknolojia ya kupambana na ukame na vumbi linalofunika anga za maeneo mmbalimbali ya Afghanistan.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 04, 2022 11:51 UTC
  • Iran: Tuko tayari kuipa Afghanistan teknolojia ya kupambana na ukame

Mjumbe wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya Afghanistan amesema kuwa, Tehran iko tayari kuipa Kabul teknolojia ya kupambana na ukame na vumbi linalofunika anga za maeneo mmbalimbali ya Afghanistan.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Hassan Kazemi Qomi  amesema hayo katika mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kuipa Afghanistan uzoefu wake na teknolojia ya kupambana na ukame na vumbi la kupindukia nchini humo.

Kwa miaka mingi sasa Afghanistan na baadhi ya nchi za eneo hili zimekumbwa na ukosefu wa mvua, ukame na kupanda hewani vumbi jingi linalofunika kabisa anga za maeneo hayo.

Wataalamu wanasema kuwa, tatizo hilo linatokana na kukauka maji katika mabwawa na mito na kutokuweko usimamiaji mzuri wa serikali katika nchi zilizokumbwa na mgogoro wa miaka mingi wa vita kama Afghanistan na Iraq.

Hassan Kazemi Qomi

 

Mjumbe maalumu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya Afghanistan amesema, Tehran inaamini kuwa, mgogoro huo wa mazingira haujali mipaka ya nchi, hivyo nchi zote za ukanda huu zinapaswa kushirikiana kupambana na jambo hilo.

Hassan Kazemi Qomi pia amesema, vumbi linalopanda hewani katika maeneo ya nchi fulani huenea pia kwenye nchi jirani na kwamba kila nchi ina jukumu la kutoa mchango wake kukabiliana na mgogoro huo. Kila mtu ana haki ya kuishi kwenye mazingira ya hali ya hewa salama na nzuri na amewataka viongozi wa Afghanistan wachukue hatua madhubuti za kufidia makosa yaliyofanywa huko nyuma na viongozi wa nchi hiyo.