Iran yasikitishwa na shambulio la kigaidi lililoua makumi Nigeria
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani shambulio la kigaidi lililoua makumi ya watu kanisani huko Nigeria hivi karibuni, sanjari na kutoa mkono wa pole kwa serikali ya Abuja na familia za raia wa nchi hiyo ambao waliuawa katika hujuma hiyo.
Katika taarifa jana Jumatatu, Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha masikitiko yake makubwa kutokana na kupoteza maisha raia wa Nigeria katika hujuma hiyo ya makundi ya kigaidi iliyolenga eneo la ibada.
Amesema jinai za namna hiyo hazikubaliki na wafuasi wa dini yoyote takatifu ya Mbinguni. Amesisitiza kuwa, misimamo ya kufurutu ada miogoni mwa wafuasi wa dini hizo inapaswa kung'olewa.
Watu zaidi ya 50 wakiwemo wanawake na watoto, waliuawa baada ya genge lenye silaha kushambulia kanisa moja la kikatoliki kaskazini magharibi mwa Nigeria wakati wa ibada ya Jumapili.
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amelaani tukio hilo na kulitaja kuwa "muaaji ya kikatili ya waumini." Amesema Nigeria katu haitasalimu amri mbele ya watu watenda maovu na kwamba hatimaye taifa la Nigeria litapata ushindi.
Hakuna genge lililotangaza kuhusika na shambulio hilo, lakini akthari ya hujuma za aina hii zimekuwa zikifanywa na wanachama wa genge la kigaidi ya Boko Haram na makundi mengine yenye mfungamano na ISIS. Nigeria imekuwa ikikumbwa na matatizo ya usalama kwa muda mrefu ambapo magaidi na magenge ya wahalifu hutekeleza mauaji kiholela.