Jenerali: Tutateketeza Tel Aviv, Haifa iwapo Israel itafanya kosa dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i84514-jenerali_tutateketeza_tel_aviv_haifa_iwapo_israel_itafanya_kosa_dhidi_ya_iran
Kamanda wa vikosi vya nchi kavu vya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameonya kuwa, Tehran itaiteketeza miji ya Tel Aviv na Haifa iwapo utawala wa Kizayuni wa Israel utajaribu kufanya kosa lolote dhidi ya taifa hili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 08, 2022 06:19 UTC
  • Jenerali: Tutateketeza Tel Aviv, Haifa iwapo Israel itafanya kosa dhidi ya Iran

Kamanda wa vikosi vya nchi kavu vya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameonya kuwa, Tehran itaiteketeza miji ya Tel Aviv na Haifa iwapo utawala wa Kizayuni wa Israel utajaribu kufanya kosa lolote dhidi ya taifa hili.

Brigedia Jenerali Kioumars Heydari amenukuliwa akisema hayo na shirika la habari la Press TV na kuongeza kuwa, "Kwa amri ya Kiongozi Muadhamu wa Mapiduzi ya Kiislamu, tutachoma moto (miji ya) Tel Aviv na Haifa hadi ibaki majivu, kwa hatua yoyote ghalati itakayochukuliwa na adui."

Amesisitiza kuwa, vikosi vya ulinzi vya Iran vimeshajiandaa kusambaratisha na kuzima ndani ya muda mfupi kabisa chokochoko itakayofanywa na mchokozi yeyote yule.

Jenerali Heydari ameeleza bayana kuwa, ardhi za Wapalestina zilizoghusubiwa na kukaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel zitakombolewa katika kipindi cha chini ya miaka 25. 

Makombora ya Iran

Ameongeza kuwa, vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran havitaruhusu mipaka na ardhi ya taifa hili vikabiliwe na hatari yoyote na vimeshajiandaa na kujiweka tayari kukabiliana na uchokozi wa aina yoyote ile.

Kadhalika Kamanda wa vikosi vya nchi kavu vya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, vikosi vya nchi kavu vimeimarisha uwezo wake wa droni na makombora; mafanikio ambayo ni mwiba kwenye jicho la adui.

Indhari hii imetolewa mwezi mmoja baada ya afisa wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kuuawa shahidi kwa kufyatuliwa risasi, mauaji yanayohusishwa na utawala khabithi wa Israel.