Kusimama kidete Iran mkabala wa ubabe na upendaji makuu wa Marekani
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuhusiana na mazungumzo ya nyuklia kwamba: Kila mara upande wa pili wa mazungumzo hayo ulipochukua mkondo wa ubabe na kutaka makuu sisi tulitumia nyenzo, nguvu na uwezo wa taifa ili wahusika watambue kwamba, maslahi na utulivu wa taifa la Iran ni jambo lenye umuhimu kwetu.
Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema siku ya Jumapili mbele ya kikao cha Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni ya Bunge la Iran na kuongeza kwamba, mkabala na muamala wa kimantiki wa upande wa pili, Jamhuri ya Kiislamu imewasilisha mapendekezo yake katika fremu ya kimantiki, ubunifu na mitazamo yake na kuifanyia kazi. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kadhalika amesema: Katika majimui ya hatua zinazochukuliwa kwa ajili ya kuzirejesha pande zote katika makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kwa jina la Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), kuna ulazima wa kuchungwa na kulindwa uwezo na nguvu za Jamhuri ya Kiislamu, matakwa yake, matarajio ya wananchi na namna ya kufatilia hayo.
Katika hali ambayo mazungumzo ya Vienna ya kuiondolea vikwazo Iran na kurejea Marekani katika makubaliano ya nyuklia takribani yamesimama kutokana na kutokuweko nia na irada ya kweli ya Washington, utawala huo wa Marekani na Troika ya Ulaya inayoundwa na mataifa ya Ujerumani, Uingereza na Ufaransa sambamba na mashinikizo ya utawala wa Kizayuni wa Israel huku Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa ya Nishati ya Atomikia (IAEA) yamepasisha azimio dhidi ya Iran katika Bodi ya Magavana ya IAEA.
Kwa hakika azimio hilo limedharau na kupuuza kikamilifu ushirikiano mpana na mkubwa wa Iran na wakala wa IAEA, ushirikiano ambao umekuwa ukifanywa na Tehran kuonyesha nia njema iliyonayo. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana Shirika la Atomiki la Iran limetangaza kuzima umeme wa camera za wakala wa IAEA nchini Iran.
Iran imeitambua hatua ya Washington na madola matatu ya Ulaya ya Uiingereza Ujerumani na Ufaransa kwamba, iko kinyume kabisa na moyo wa kidiplomasia na kutahadharisha kwamba, hatua yoyote yenye matashi ya kisiasa ndani ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) itakabiliwa na jibu mwafaka, athirifu na la haraka la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Licha ya kuwa baada ya kupasishwa azimio hilo, serikali ya Marekani imedai kwamba, ingali inafuatilia suala la kurejea kwake katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, lakini hatua iliyochukuliwa dhidi ya Iran inaonyesha kuwa, upande wa Magharibi katika mazungumzo ya nyuklia unatumia azimio lenye matashi ya kisiasa la Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kama wenzo wa mashinikizo dhidi ya Iran na kufidia mkwamo wa sasa uliojitokeza katika mazungumzo ya Vienna.
Kwa maneno mengine ni kuwa, filihali Marekani haina wenzo mwingine wowote ambao inaweza kuutumia kwa ajili ya kuishinikiza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ndio maana imeamua kuutumia vibaya wakala wa IAEA na masuala ya kiufundi na hivyo kuongeza kiwango chake cha kutaka ipatiwe upendeleo na kwa msingi huo iilazimishe Iran irejee nyuma na kulegemeza misimamo kuhusiana na matakwa yake ya kisheria.
Mazungumzo ya Vienna yamesimama kutokana na serikali ya Rais Joe Biden wa Marekani ambayo kinyume na ilivyokuwa ikikosoa sera zilizogonga mwamba za Donald Trump haijawa tayari kubadilisha sera hizo na kuondoa vikwazo sambamba na kuipatia Iran dhamana yenye itibari ya utekelezwaji wa tangazo la kuondolewa vikwazo. Hivi sasa sharti la kuhuishwa mazungumzo hayo na Marekani kukubaliwa tena uanchama katika makubaliano ya nyuklia ni kudhaminiwa maslahi ya Iran.
Mintarafu hiyo, kuiwekea mashinikizo yenye wigo mpana Jamhurii ya Kiislamu ya Iran ni jambo ambalo katu halitakuwa na msaada wowote wa haraka kwa kadhia ya JCPOA, bali hilo litazidi kuifanya hali ya mambo kuwa tata zaidi na kuandaa uwanja wa kuibukka changamoto mpya.
Hapana shaka kuwa, kudumishwa vikwazo, kupasishwa azimio katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na kutumiwa siasa za kindumakuwili katika udiplomasia sambamba na mashinikizo ya kiwando cha juu kabisa ya Marekani dhidi ya Iran, siyo tu kwamba, hayajengi hali ya kuaminiana kwa upande wa Washington, bali kwa mara nyingine tena yanadhihirisha sifa ya ubabe na kupenda makuu iliyonayo White House katika mazungumzo.
Hii ni katika hali ambayo, Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Tehran katu haitasalimu amri mbele ya ubabe na upendaji makuu wa upande wa pili.