Iran yamuonya mkuu wa IAEA asifanye 'mambo kuwa magumu'
Msemaji wa Shirika la Atomiki la Iran amemshauri Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) kujizuia kufanya mambo kuwa magumu kwa kutoa matamshi ya kisiasa.
Behrouz Kamalvandi ametoa onyo hilo Jumatano baada ya Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA kutoa wito kwa Iran kuanzisha mazungumzo haraka kuhusu kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA ya mwaka 2015 kabla hali kuwa ya 'matatizo zaidi'.
Katika kujibu, Kamalvandi amesema: "Namshauri Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA ajiweke mbali na matamshi yasiyo ya kitaalamu yenye rangi ya kisiasa na yanayokusudiwa kwa vyombo vya habari."
Msemaji wa Shirika la Atomiki la Iran amesema iwapo kuna suala la kiufundi linapaswa kushughulikiwa kitaalamu katika fremu ya majukumu ya IAEA kupitia njia za kawaida za shirika hilo la Umoja wa Mataifa la nishati ya atomiki.
Kamalvandi alikuwa akiashiria mahojiano ambayo Grossi aliyafanya hivi karibuni na televisheni ya CNN ya Marekani ambapo alitoa matamshi yenye uhasama usio wa kawaida dhidi ya Iran.
Grossi aliibua utata hivi karibuni alipofika katika utawala wa Kizayuni wa Israel na kukutana na wakuu wa utawala huo mwezi jana.
IAEA imekuwa ikikosolewa kwa kupokea nyaraka kutoka Israel kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, nyaraka ambazo Iran inasisitiza ni bandia kwani zimetolewa kwa ushirikinao na kundi la kigaidi la MKO.
Baada ya safari hiyo ya Grossi huko Israel, Bodi ya Magavana wa IAEA ilipitisha azimio ikiituhumu Iran kuwa haishirikiani na wakala huo madai ambayo Iran imeyapinga.
Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran AEOI limetangaza kuwa hakuna mada yoyote ya nyuklia nchini ambayo haijatolewa maelezo; na madai ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA yametokana na taarifa zisizo sahihi na za kubuni ulizopewa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ambao wenyewe unamiliki silaha za nyuklia.