Kamal Kharrazi: Iwapo Iran itashambuliwa, tutapiga ndani kabisa ya utawala wa Kizayuni
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i85992-kamal_kharrazi_iwapo_iran_itashambuliwa_tutapiga_ndani_kabisa_ya_utawala_wa_kizayuni
Mkuu wa Baraza la Kistratijia la Mahusiano ya Kigeni la Iran amesema: Iwapo vituo nyeti vya Iran vitashambuliwa tutalenga ndani kabisa ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 18, 2022 02:31 UTC
  • Kamal Kharrazi: Iwapo Iran itashambuliwa, tutapiga ndani kabisa ya utawala wa Kizayuni

Mkuu wa Baraza la Kistratijia la Mahusiano ya Kigeni la Iran amesema: Iwapo vituo nyeti vya Iran vitashambuliwa tutalenga ndani kabisa ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kamal Kharrazi ameyasema hayo katika mahojiano yake na Televisheni ya Al Jazeera ya Qatar na kuongeza kuwa: Taarifa ya Quds (hati ya pamoja kati ya Marekani na utawala wa Kizayuni ambayo ilitiwa saini baada ya ziara ya Biden katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina), ni taarifa ya kukaririwa tu na haitakuwa na matokeo yoyote.

Waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje wa Iran amesisitiza kuwa: Utawala wa Kizayuni wa Israel uko katika hali dhaifu na uungaji mkono wa Joe Biden kwa utawala huo hautabadilisha chochote.

Afisa huyo wa ngazi za juu wa Iran ameongeza kuwa: Shambulio lolote dhidi ya usalama wa Iran kutoka nchi jirani litakabiliwa na jibu kali la Iran kwa nchi hizo, na jibu la moja kwa moja kwa utawala wa Kizayuni.

Kamal Kharrazi

Rais Joe Biden wa Marekani na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Yair Lapid, Jumatano iliyopita walitia saini "Taarifa ya Pamoja ya Quds" wakati wa ziara ya Biden katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina na kusisitiza haja ya kuendelezwa uhusiano zaidi kati ya utawala wa Tel Aviv na nchi za Kiarabu.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, Washington bado ina dhamira ya dhati ya kulinda usalama wa utawala wa Israel na kuhakikisha kwamba utawala huo unakua na nguvu kubwa zaidi za kijeshi katika eneo la Magharibi mwa Asia. Vilevile imesisitiza kuwa Washington haitairuhusu Iran kupata silaha za nyuklia, na kwamba Marekani iko tayari kutumia uwezo wake wa kitaifa kuhakikisha suala hilo.