Iran yalaani mauaji ya raia wa Iraq, Uturuki yakanusha kuhusika na shambulio
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i86140-iran_yalaani_mauaji_ya_raia_wa_iraq_uturuki_yakanusha_kuhusika_na_shambulio
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani shambulio lililofanywa katika mji wa Zakho na kusisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono kikamilifu uthabiti na usalama wa Iraq.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 22, 2022 02:36 UTC
  • Iran yalaani mauaji ya raia wa Iraq, Uturuki yakanusha kuhusika na shambulio

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani shambulio lililofanywa katika mji wa Zakho na kusisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono kikamilifu uthabiti na usalama wa Iraq.

Hossein Amir- Abdollahian ametoa sisitizo hilo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu Alkhamisi na waziri mwezake wa Iraq Fuad Hussein na kulaani shambulio dhidi ya mji wa kitalii wa Zakho ulioko kwenye jimbo la Dohuk katika mpaka wa pamoja wa Uturuki na eneo la Kurdistan ya Iraq.

Shambulio hilo limelenga umati wa watu wakiwemo wanawake na watoto waliokuwa wamejumuika na familia zao kwa ajili ya kuburudika katika mandhari za kimaumbile za eneo hilo la kitalii.

Mbali na kuzipa pole na kuzifariji familia za waathirika wa shambulio hilo pamoja na serikali na wananchi wa Iraq, Amir-Abdollahian ametilia mkazo uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu kwa uthabiti na usalama wa Iraq.

Duru za habari za Iraq zilitangaza Jumatano kuwa, jeshi la Uturuki limeshambulia kwa mizinga kaskazini ya nchi hiyo na kulenga mji wa kitalii wa Zakho katika eneo la Kurdistan na kusababisha watu 11 kuuawa, wakiwemo watoto na wanawake na wengine 31 kujeruhiwa.

Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al Kadhimi

Wakati duru za Iraq zinasisitiza kuwa jeshi la Uturuki ndilo lililohusika na shambulio hilo katika mji wa Zakho, serikali ya Ankara imekanusha tuhuma hizo na kudai kwamba wapiganaji wa Chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan P.K.K ndio waliohusika na hujuma hiyo.

Hata hivyo P.K.K imetoa taarifa ikisisitiza kwamba, haina mpiganaji hata mmoja katika eneo lilikotokea shambulio la Jumatano na kwamba eneo hilo linakaliwa na wanajeshi wa Uturuki.

Kufuatia shambulio la siku ya Jumatano ndani ya ardhi ya Iraq, Waziri Mkuu wa nchi hiyo Mustafa al-Kadhimi alitangaza jana Alkhamisi kuwa siku ya maombolezo ya nchi nzima na mbali na kuihusisha Uturuki na shambulio katika mji wa Zakho amesisitiza kuwa Iraq inalinda ina haki kamili ya kujibu uchokozi uliofanywa dhidi yake na itachukua hatua zinazohitajika kuwalinda watu wake na kuhakikisha upande ulioanzisha uchokozi unabeba dhima ya mivutano ya kila mara unayoanzisha.

Wakati huohuo ripoti kutoka Iraq zinasema, Baraza la Usalama wa Taifa la nchi hiyo limefanya kikao cha dharura na kupitisha uamuzi wa kutaka balozi wa Uturuki nchini humo aitwe, serikali ya Ankara iombe ardhi kwa shambulio la Jumatano na vilevile iwaondoe wanajeshi wake katika ardhi ya Iraq.../