Iran kurusha satalaiti katika anga za mbali karibuni hivi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i86200-iran_kurusha_satalaiti_katika_anga_za_mbali_karibuni_hivi
Mkuu wa Shirika la Anga za Mbali la Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu katika miezi michache ijayo itarusha satalaiti katika anga za mbali.
(last modified 2026-05-06T11:35:21+00:00 )
Jul 23, 2022 06:54 UTC
  • Iran kurusha satalaiti katika anga za mbali karibuni hivi

Mkuu wa Shirika la Anga za Mbali la Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu katika miezi michache ijayo itarusha satalaiti katika anga za mbali.

Hassan Salarieh amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la IRIB na kuongeza kuwa, satalaiti hiyo inatazamiwa kurushwa katika anga za mbali katika msimu wa mapukutiko hapa nchini.

Amesisitiza kuwa, taifa lolote lile katika dunia ya leo linapaswa kuwa amilifu katika uga wa anga za mbali, vinginevyo mamlaka kamili ya kujitawala nchi huenda isipatikane kwa kupuuzwa sekta hii.

Salarieh amesema kuendesha na kusimamia sekta ya kilimo kunahitaji programu za anga za mbali, na bila mikakati hiyo, ukulima utakuwa na gharama za juu kupindukia.

Satalaiti ya kijeshi ya Nour- 1 iliyorushwa angani miaka 2 iliyopita

Amesema kujirushia satalaiti katika anga za mbali kwa kutegemea wataalamu wa ndani ya nchi kuna maana kuwa, Iran hii leo imeweza kuwashinda maadui na kumiliki teknolojia muhimu na za kisasa licha ya vikwazo na mashinikizo.

Ikumbukwe kuwa, Machi mwaka huu, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilitangaza kuwa limerusha kwa mafanikio makubwa satalaiti ya kijeshi iliyopewa jina la Nour-2 katika anga za mbali.