Jul 27, 2022 03:02 UTC
  • Karibuni hivi Ugiriki itarejesha shehena ya mafuta ya Iran iliyoiba

Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Ugiriki umetangaza kuwa operesheni ya kuyahamisha na kuyarejesha mafuta ya Iran yaliyoibwa itaanza hivi karibuni.

Tarehe 25 Mei mwaka huu na kwa agizo la Marekani, Ugiriki ilichukua hatua ya kuikamata na kuizuia meli ya mafuta ya Kirusi ya Lana iliyokuwa imebeba mapipa laki saba ya mafuta ya Iran.

Serikali ya Ugiriki ilikiri kuwa, uamuzi wa kuzuia shehena hiyo ya mafuta ya Iran ulitokana na takwa la wizara ya fedha ya Marekani, lakini haikubainisha kwa nini nchi hiyo iliamua kutekeleza agizo hilo la Washington.

Hatua hiyo iliyochukuliwa na serikali ya Athens ililalamikiwa vikali na viongozi wa Iran wakisisitiza kwamba kitendo hicho ni uharamia wa baharini.

Kutokana na mashinikizo yaliyoendelea kutolewa na serikali ya Iran hatimaye Ugiriki ilikubali kuyaachia mafuta ya Iran na mahakama ya nchi hiyo ikatoa hukumu ya kubatilisha uzuiaji meli ya mafuta ya Kirusi.

Shirika la habari la Iran Press limeripoti kuwa ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Athens umetangaza katika ujumbe uliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter ya kwamba: Mahakama ya Juu ya Ugiriki, ambayo ndicho chombo cha juu kabisa cha Idara ya Mahakama ya nchi hiyo imethibitisha hukumu iliyotolewa na mahakama ya rufaa kwa manufaa ya Iran na kwamba karibuni hivi operesheni ya kuhamisha na kuyarejesha kwenye meli ya Lana mafuta ya Iran yaliyoibwa itaanza kutekelezwa.../

Tags