Raisi: Iran haitafungamanisha ustawi wake na mazungumzo ya JCPOA
(last modified Sat, 13 Aug 2022 11:25:40 GMT )
Aug 13, 2022 11:25 UTC
  • Raisi: Iran haitafungamanisha ustawi wake na mazungumzo ya JCPOA

Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislami katu haitafungamanisha ustawi wake na mazungumzo ya kujaribu kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Rais Raisi alisema hayo jana Ijumaa katika mkoa wa Kerman, kusini mashariki mwa nchi na kuongeza kuwa, kamwe taifa hili halitayahusisha maendeleo ya nchi na utatuzi wa matatizo na suala la mapatano ya JCPOA.

Kadhalika amesisitiza kuwa, timu ya mazugumzo ya kuiodolea Iran vikwazo vya kidhalimu haitaondoka kwenye meza ya mazungumzo. Duru mpya ya mazungumzo ya uondoaji vikwazo vya kidhalimu ilivyowekewa Iran ilianza mjini Vienna, Austria Alkhamisi ya tarehe 4 Agosti.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, Iran haiwezi kusitisha mchakato wake wa ustawi kutokana na vikwazo na mashinikizo.

Kikao cha Vienna

Sayyid Raisi ameeleza bayana kuwa, "mkondo wetu wa ustawi na maendeleo hauwezi kusitishwa na vikwazo na mashinikizo. Hatutakubali maadui wafanikishe malengo yao, ambayo ni kulemaza uzalishaji na kusambaratisha ucumi na utamaduni wa Iran."

Amesema serikali yake itaendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto za kiuchumi na kiutamaduni zinazolikabili taifa hili, pasi na kuzingatia mkondo utakaochukuliwa na mazungumzo ya kufufua JCPOA.

Rais wa Iran amefafanua zaidi kwa kusema: Pamoja na azma ya maadui, lakini masuala ya Iran yatafuatiliwa kwa kuwashirikisha wananchi na wasomi, na mustakabali wa taifa utakuwa na mwanga.