Nov 24, 2025 03:00 UTC
  • Leo Katika Historia
    Leo Katika Historia

Leo ni Jumatatu 03 Jamadithani 1447 Hijria ambayo inasadifiana na 24 Novemba 2025.

Siku kama ya leo miaka 1436 iliyopita alikufa shahidi Bibi Fatima al Zahra, binti mtukufu wa Mtume wetu Muhammad (saw) na mke wa Imam Ali bin Abi Twalib (as).

Alizaliwa miaka mitano baada ya kubaathiwa Nabii Muhammad (saw) na mtukufu huyo akampa jina la Fatima. Alipewa malezi na wazazi wake wawili yaani Bibi Khadija na Mtume wa Mwenyezi Mungu na kupata maarifa aali ya dini kutoka kwa baba yake. Bibi Fatima alifikia daraja za juu za ukamilifu wa kiroho na kimaanawi ndani ya nyumba ya wahyi na ufunuo.

Baada ya kuolewa na Imam Ali bin Abi Twalib ambaye alikuwa kielelezo halisi cha takwa na uadilifu, Bibi Fatima alikuwa na nafasi kubwa na alitoa mchango wa aina yake katika jamii ya Kiislamu. Alikuwa dhihirisho la uchamungu, ukarimu, kujitolea, subira, kujipinda katika ibada na kuwasaidia watu wote na alilea watu adhimu kama Imam Hassan na Hussein (as).

Katika siku kama ya leo miaka 788 iliyopita, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria alifariki dunia Abu Bakr Muhammad bin Ahmad maarufu kwa jina la Ibn Sayyidun-Naas, faqihi, mtaalamu wa hadithi, mwanahistoria na msomi wa fasihi wa Andalusia au Hispania ya leo.

Mwanazuoni huyo alifariki dunia nchini Tunisia. Ibn Sayyidun-Naas alizaliwa mwaka 597 Hijiria katika viunga vya mji wa Seville (Ishbilia) huko Uhispania na kuanza kujishughulisha na masomo. Abu Bakr Muhammad bin Ahmad alifundisha kwa miaka mingi katika eneo hilo na kulea wanafunzi wengi.

Msomi huyo alitabahari pia katika taaluma ya mashairi na fasihi; na mashairi yake mengi yanamsifu Mtume Muhammad (saw). Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni kile cha Sira na Maisha ya Mtume Muhammad (saw).

Siku kama ya leo miaka 393 iliyopita, alizaliwa Baruch de Spinoza mwanafalsafa na mtaalamu wa elimu jamii wa Uholanzi.

Spinoza alisoma kwa bidii na kukwea daraja za kielimu. Hata hivyo ukosoaji wake wa dini ya Kiyahudi ulimfanya akabiliwe na chuki na uhasama wa maulama wa dini hiyo.

Njia na fikra za kifalsafa za Spinoza zilikaribiana na itikadi za kisufi. Msomi huyo wa elimu ya falsafa wa Uholanzi ameandika pia vitabu kadhaa kama The Philosophy of Spinoza na The Road to Inner Freedom. Baruch de Spinoza alifariki dunia mwaka 1677.   

Katika siku kama ya leo miaka 194 iliyopita, Michael Faraday mwanafizikia stadi wa Kiingereza aligundua mkondo wa umeme unaojulikana kitaalamu kama ''Electric Current''.

Kwa ugunduzi huo Faraday akawa amefanikiwa kupiga hatua kubwa katika elimu ya fizikia. Faraday alizaliwa mwaka 1791 na awali alikuwa akifanya kazi katika duka la kuuza vitabu. Ni kipindi hicho ndipo taratibu alipoanza kusoma vitabu mbalimbai na kuanza kuvutiwa na masuala ya kielimu. Miaka michache baadaye akawa msaidizi wa maabara.

Akiwa katika maabara hiyo Faraday alifanya utafiti mwingi kuhusiana na jinsi ya kutengeneza balbu za umeme. Miongoni mwa mafanikio mengine makubwa yaliyoletwa na mtaalamu huyo ni pale alipogundua mota ya umeme pamoja na kubadilisha nguvu za sumaku kuwa nguvu za umeme.   

Katika tarehe kama ya leo miaka 161 iliyopita, alizaliwa mchoraji na msanii mkubwa wa Ufaransa, Henri Toulouse Lautrec. Familia ya Lautrec ilikuwa ya kipato cha wastani na licha ya kukabiliwa na matatizo mengi ya kimaisha, Lautrec alitokea kuwa miongoni mwa wasanii mashuhuri na hodari wa Ufaransa kutokana na kipawa chake kikubwa. Msanii huyo alifariki dunia mwaka 1901. 

Miaka 119 iliyopita katika siku kama ya leo ambayo ni sawa na tarehe 3 Azar mwaka 1285 Hijria Shamsia, gazeti la 'Majlis' lililokuwa na kurasa 8 lilianza kuchapishwa nchini Iran.

Mhariri Mkuu wa gazeti hilo alikuwa Adib al Mamalik Farahani ambaye alikuwa miongoni mwa waandishi mashuhuri wa zama hizo.

Mbali na gazeti hilo kuandika habari za ndani na nje ya nchi, liliakisi pia mazungumzo yote ya Majlisi ya Ushauri yaani Bunge la Iran.   

Na siku kama ya leo miaka 12 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi 6 zinazounda kundi la 5+1 zilitia saini makubaliano ya muda ya nyuklia mjini Geneva huko Uswisi.

Kutiwa saini makubaliano hayo kulitayarisha uwanja mzuri na kufungua njia ya mazungumzo zaidi kati ya Iran na nchi hizo sita ambazo ni Marekani, Ufaransa, Uingereza, Russia, China na Ujerumani kwa ajili ya kutia saini makubaliano kamili ya nyuklia na kuondoa hitilafu kuhusu miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia hapa nchini, na mwishowe kufutwa vikwazo vya kidhalimu vilivyowekwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.