Momeni: Iran inaongoza nchi zote duniani kwa kukamata madawa ya kulevya
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i87238-momeni_iran_inaongoza_nchi_zote_duniani_kwa_kukamata_madawa_ya_kulevya
Katibu Mkuu wa Kamati ya Kupambana na Madawa ya Kulevya ya Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ndiyo nchi inayokamata kiwango kikubwa zaidi cha mihadarati na madawa ya kulevya duniani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 20, 2022 10:08 UTC
  • Momeni: Iran inaongoza nchi zote duniani kwa kukamata madawa ya kulevya

Katibu Mkuu wa Kamati ya Kupambana na Madawa ya Kulevya ya Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ndiyo nchi inayokamata kiwango kikubwa zaidi cha mihadarati na madawa ya kulevya duniani.

Shirika la habari la Iran Press limemnukuu Brigedia Jenerali wa Polisi, Eskandar Momeni akisema hayo leo Jumamosi mbele ya waandishi wa habari na huku akigusia siasa za kamati yake hiyo za kupambana na mihadarati amesema, vita dhidi ya madawa ya kulevya haviwezekani bila ya kushirikishwa kikamilifu wananchi na kwamba inabidi uwezo wote uliopo utumike kwa ajili ya kupambana na madawa hayo haramu.

Katibu Mkuu huyo wa Kamati ya Kupambana na Madawa ya Kulevya ya Iran pia amesema, kinga ni bora kuliko tiba, na kwamba suala la kukinga ndilo linalopewa kipaumbele zaidi na kamati yake. Amesema, Iran ina mpaka mkubwa na Afghanistan na ndio maana wafanyamagendo wa madawa ya kulevya wanapenda kutumia ardhi ya Iran katika magendo yao.

Wanajeshi wa Marekani katika mashamba ya mihadarati nchini Afghanistan

 

Pia amesema, katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, wakati Afghanistan ilipokuwa inakaliwa kwa mabavu na wanajeshi wa Marekani, kiwango cha uzalishaji mihadarati kiliongezeka mara 20 huko Afghanistan na kufikia tani 9,500 kwa mwaka.

Brigedia Jeneli Momeni pia amesema, Iran inakamata asilimia 90 ya madawa ya kulevya aina ya tiryak, asilimia 48 ya morphine na asilimia 26 ya heroine duniani. Vile vile amesema, Iran ni amilifu (active) sana katika mapambano dhidi ya mihadarati kwenye taasisi za kimataifa na inashirikiana vizuri na nchi nyingine katika vita dhidi ya madawa ya kulevya.