Iran inazalisha asilimia 98 ya dawa zake ndani ya nchi
Shirika la Dawa na Chakula la Iran (FDA) limesema asilimia 98 ya dawa zilizoko nchini zinazalishwa na wataalamu wa taifa hili, na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ni miongoni mwa nchi 20 duniani zinazojizalishia dawa kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu.
Bahram Daraei, Mkuu wa Shirika la Dawa na Chakula la Iran amesema hayo leo Jumamosi katika mahojiano na kueleza kuwa, mafanikio haya yamepatikana licha ya mifumo ya dawa na matibabu ya Jamhuri ya Kiislamu kuwa chini ya vikwazo.
Daraei amenukuliwa na shirika la habari la IRNA akisema hayo na kuongeza kuwa, Marekani inaihadaa dunia kwamba vikwazo vyake havilengi bidhaa za kibinadamu kama dawa.
Afisa huyo wa Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema taifa hili lilifanikiwa kuzalisha aina sita za chanjo ya kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO-19, na kwa utataribu huo likafanikiwa pakubwa dhidi ya janga la Corona ambalo linaendelea kusumbua baadhi ya nchi mpaka sasa.

Kadhalika amepongeza mfumo wa afya wa nchi hii, ambao uliundwa na serikali kwa ajili ya kusimamia usambazaji wa dawa kote nchini, jambo ambalo limesaidia kudhibiti magendo ya dawa.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza kuwa, vikwazo vya Marekani vinazuia kufikishwa vifaatiba, dawa, teknolojia na ushirikiano wa Iran na taasisi za kifedha za kimataifa, na kuitaja jinai hiyo kama ugaidi wa kimatibabu.