Ebrahim Raisi: Wapalestina ndio wenye haki ya kuishi katika ardhi za Palestina
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, wananchi wa Palestina ndio wenye haki ya kujiamulia wenyewe mustakbali wao na ndio wenye haki ya kuishi katika ardhi hizo.
Rais Raisi amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na kipindi cha "Dakika 60" cha televisheni ya CBS ya Marekani ambayo yamerushwa hewani mapema leo asubuhi na kuongeza kuwa, wananchi wa Palestina ni uhakika usiokanushika ambao hivi sasa wamefukuzwa katika ardhi zao za asili na wanaishi ukimbizini kwa mamilioni. Amesema, ni uhakika usiopingika pia kuwa, utawala wa Kizayuni ni utawala pandikizi unaoishi katika ardhi walizoporwa wenye asili ya Palestina yaani wananchi wenyewe wa ardhi hizo.
Pia amesema, nchi ambazo leo zinaweka uhusiano wa kawaida na Israel, ni washiriki wa jinai za utawala huo katili dhidi ya Wapalestina.
Rais Ebrahim Raisi aidha amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuwa, makubaliano yoyote yasiyo na dhamana hayana maana hasa kutokana na tabia ya Marekani ya kutoheshimu ahadi na mikataba hata inayoitia saini yenyewe.
Iran haitetereki katika msimamo wake wa kupatikana mapatano mazuri na yenye uhakika wa kutekelezwa. Inabidi makubaliano hayo yawekewe misingi mizuri na madhubuti ili Marekani isiweze kujitoa tena.
Amesema, Marekani ina historia ya kutoheshimu mikataba yake. Sasa upande wa pili unapokuwa na tabia hizo za kutoheshimu mapatano; makubaliano yasiyo na dhamana yana maana gani?
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amesisitiza kuwa, Tehran haiwezi kuiamini Marekani kwani tayari ina uzoefu mchungu wa usaliti na kutoheshimu ahadi zao viongozi wa Washington.
Akitoa ufafanuzi kuhusu umuhimu wa nishati ya atomiki kwa matumizi ya amani, Rais Ebrahim Raisi amsema: Nishati ya nyuklia ina matumizi mengi katika masuala ya tiba, kilimo, mafuta na gesi.
Amma kuhusu jinai ya Marekani ya kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, kamanda wa zamani wa Kikosi cha Quds, cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, amesema, kitendo cha serikali iliyopita ya Marekani na hasa rais wa wakati huo Donald Trump cha kutoa amri ya kuuliwa kidhulma Luteni Jenerali Qassem Soleimani ni jinai iliyo dhidi ya ubinadamu.