Msisitizo mwingine wa Iran wa kuwa tayari kubadilishana wafungwa na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i88348-msisitizo_mwingine_wa_iran_wa_kuwa_tayari_kubadilishana_wafungwa_na_marekani
Nasser Kanaani, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi karibuni alitembelea shirika la habari la ISNA ambapo pamoja na mambo mengine alifanyiwa mahojiano maalumu na ripota wa shirika hilo lililopo jijini Tehran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 19, 2022 21:51 UTC
  • Msisitizo mwingine wa Iran wa kuwa tayari kubadilishana wafungwa na Marekani

Nasser Kanaani, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi karibuni alitembelea shirika la habari la ISNA ambapo pamoja na mambo mengine alifanyiwa mahojiano maalumu na ripota wa shirika hilo lililopo jijini Tehran.

Moja ya masuali aliyoulizwa ni: "katika mambo yanayojadiliwa pembeni ya mazungumzo ya kufufua makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni mabadilishano ya wafungwa kati ya Iran na Marekani. Kwa vile inavyooonekana kwa kiwango fulani matumaini ya kufufuliwa JCPOA yameshafifia, suala hilo la kubadilishana wafungwa baina ya Iran na Marekani litakuwaje? Au na hilo pia limeshaondolewa?
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alieleza kuhusiana na suala hilo kwamba, "tulipotangaza kuwa suala la kubadilishana wafungwa halina uhusiano wowote na mchakato wa JCPOA, maana yake ni kwamba, kwa kuwepo au kutokuwepo JCPOA, sisi tuko tayari kutatua suala la wafungwa, kwa kuwa ni kadhia ya kibinadamu. Sasa hivi uamuzi ni wa serikali ya Marekani kutekeleza mabadilishano hayo au la."
Nasser Kanaani

Kanaani alifafanua zaidi kwa kusema: "sisi tulitangaza hapo kabla kuwa tuko tayari kubadilishana wafungwa na tungali tuna utayari huo. Kuhusiana na suala hili, yamefanyika mazungumzo kupitia njia tofauti; na pande mbili zimefikia makubaliano yanayohitajika; na hivi sasa uamuzi ni wa serikali ya Marekani kutekeleza makubaliano hayo au la. Sisi tuko tayari kutekeleza makubaliano hayo."

Iran imetangaza tena kuwa iko tayari kubadilishana wafungwa na Marekani kutokana na kuwepo idadi kadhaa ya wafungwa katika magereza ya nchi hizo mbili wanaoshikiliwa kwa sababu na kwa tuhuma mbalimbali. Marekani imedai mara kadhaa kuwa iko tayari kubadilishana wafungwa, lakini kila wakati imekwepa kufanya hivyo kwa kisingizio hiki na kile.
Wafungwa ambao Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka waachiliwe huru wameshtakiwa na kuhukumiwa kwa tuhuma zinazohusiana na ukiukaji vikwazo ilivyowekewa Iran na Marekani. Kwa upande mwingine, kuna idadi kadhaa ya watu wenye uraia wa Iran na Marekani ambao wamefungwa jela Iran kwa makosa mbalimbali, na ambao Iran haiutambui uraia wao wa kigeni.
Hapo awali, na katika kuendesha vita vya kisaikolojia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, baadhi ya vyombo vya habari vya Magharibi vilidai kwamba Tehran inajaribu kuhusisha suala la kuachiliwa huru wafungwa na kupigwa hatua au kufikia natija mazungumzo ya Vienna ya uondoaji vikwazo, ilhali Iran ilishatangaza mara kadhaa kwamba, suala hilo halina uhusiano wowote na mazungumzo ya JCPOA na kwamba Tehran imejipanga kikamilifu kutekeleza zoezi la kubadilishana wafungwa.
Mabadilishano ya wafungwa yaliyowahi kufanywa kati ya Iran na Marekani

Katika mkutano wake na waandishi wa habari aliofanya tarehe Agosti 17, Kanaani alisema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, bila ya kuhusisha na JCPOA, imeitangazia mara kadhaa Marekani utayari wake wa kushughulikia suala la wafungwa kwa kupitia njia mbalimbali." Sambamba na kuashiria mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yaliyofanyika kati ya nchi mbili kuhusiana na kubadilishana wafungwa, Kanaani aliongezea kuwa Iran imeshatangaza mara kadhaa kuwa iko tayari "kutekeleza haraka makubaliano yaliyopo" kuhusu wafungwa.

Lakini mkabala wake, serikali ya Biden imeonyesha misimamo inayokinzana juu ya suala hilo. Marekani imeituhumu Tehran kwamba inatekeleza sera ya ushikiliaji mateka na kutafuta kikomboleo kwa mabavu kuhusiana na kufungwa jela baadhi ya Wairan wenye uraia wa kigeni, ilhali uhalifu na makosa yaliyofanywa na watu hao umebainishwa wazi.
Mnamo katikati ya mwezi uliopita wa Agosti, Robert Malley, mwakilishi maalum wa Marekani katika masuala ya Iran, aliituhumu Iran kwa kile alichodai, kutumia vibaya kama silaha ya kisiasa kile alichokiita kuwapa "kifungo kisicho cha uadilifu" raia wa Marekani.
Na hii ni katika hali ambayo, Marekani imewafunga jela raia kadhaa wa Iran kwa kisingizio cha kukiuka vikwazo au kujaribu kusafirisha bidhaa au vifaa ambayo Iran imesusiwa kuuziwa, huku ripoti zikionyesha kuwa raia hao hawatendewi inavyostahiki na wanakabiliwa na hali na mazingira magumu katika magereza ya Marekani wanakoshikiliwa.

Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani kuhusu kubadilishana wafungwa yalishafanyika hapo kabla pia; na mazungumzo zaidi yamefanyika juu ya suala hilo kupitia muunganishi tangu yalipoanza tena mazungumzo ya Vienna ya uondoaji vikwazo.

Saeed Khatibzadeh, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wakati huo, mnamo tarehe 7 Machi mwaka huu alisema: Iran na Marekani zimepiga hatua katika mazungumzo ya kubadilishana wafungwa, na iwapo Marekani itatekeleza wajibu na ahadi zake, faili hilo linaweza kuhitimishwa.
Lakini licha ya matamshi hayo ya matumaini yaliyotoka upande wa Iran, Washington, kama ilivyo katika masuala mengine mengi, imeamua kufuata sera tatanishi; na kimsingi ni kwamba haijachukua hatua au kufanya juhudi zozote za maana kuhusiana na ubadilishanaji na kuachiwa huru wafungwa wa pande mbili.../