Balozi wa Denmark aitwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran
Oct 07, 2022 23:34 UTC
Balozi wa Denmark mjini Tehran ameitwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kufuatia shambulio lililofanywa dhidi ya ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Denmark na mshambuliaji aliyekuwa amebeba silaha baridi.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, kufuatia shambulio lililofanywa jana Ijumaa dhidi ya ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Copenhagen na mtu aliyekuwa amebeba silaha baridi, ambaye alitoa vitisho kwa balozi wa Iran, akamjeruhi mfanyakazi mmoja raia wa Denmark na kuharibu pia magari ya ubalozi huo, balozi wa Denmark hapa mjini Tehran alitakiwa jana hiyohiyo kufika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran.

Katika mkutano na balozi huyo, Mkurugenzi Mkuu wa Ulaya Magharibi wa wizara ya mambo ya nje ya Iran aliwasilisha malalamiko rasmi kwa balozi huyo wa Denmark kutokana na serikali yake kushindwa kudhamini usalama wa ubalozi wa Iran na wanadiplomasia wake.
Katika mkutano huo ilisisitizwa pia kwamba, kwa mujibu wa Mkataba wa Vienna, wajibu wa serikali mwenyeji katika suala hilo umebainishwa kwa uwazi kabisa, na kwa hivyo inatarajiwa kuwa serikali ya Denmark itatekeleza majukumu iliyonayo kimataifa kuhusu kudhamini usalama wa maeneo ya kidiplomasia.
Kwa upande wake, balozi wa Denmark ameomba radhi kwa tukio lililotokea na akasisitiza kuwa, baada ya kujiri tukio hilo, hatua za usalama zitaimarishwa zaidi na atawasilisha haraka kwa serikali ya Copenhagen taarifa ya malalamiko ya Iran.../
Tags